Jumapili tarehe 20 Novemba 2022
Leo ni Jumapili tarehe 25 Rabiuthani 1444 Hijria sawa na 20 Novemba 2022.
Mwaka 288 Hijiria katika siku kama ya leo miaka 1156 iliyopita, alifariki dunia Thabit bin Qurrah Swabi, mtaalamu wa hesabati, nyota na tabibu katika kipindi cha utawala wa Bani Abbas. Alizaliwa mwaka 221 Hijiria, mjini Harran Mesopotamia nchini Iraq. Thabit bin Qurrah Swabi alikuwa akizungumza lugha za Kigiriki, Kiasyria na Kiarabu. Alisafiri kwenda mjini Baghdad Iraq kwa lengo la kusoma na kwa usimamizi wa Muhammad bin Musa aliyekuwa mtaalamu mkubwa Mwislamu wa hesabati na nyota kipindi hicho, Thabit bin Qurrah Swabi akaingia katika uwanja wa elimu hizo. Aliwasilisha nadharia mpya katika uwanja wa hesabati. Aidha katika utaalamu wa nyota yeye ni katika watu wa kwanza kurekebisha chombo cha Ptolemaic. Thabit bin Qurrah Swabi aliandika vitabu vingi katika uwanja wa tiba, hesabati na nyota, vilivyofasiriwa kutoka lugha ya Kigiriki kwenda Kiarabu, miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Adh Dhakhiratu Fii Ilmi al Twib" na "Kitabul Mafrudhat."
Miaka 1076 iliyopita mwaka 368 Hijria, alizaliwa mjini Corduba, (Qurtuba) Uhispania, faqih mtaalamu wa hadith, fasihi na mwanahistoria Abu Omar Yusuf bin Abdallah mashuhuri kwa jina la Abdul Birr. Alipata masomo ya msingi kutoka kwa baba yake na walimu wengine wakubwa wa kipindi hicho. Ibnu Abdul Birr aliupa umuhimu mkubwa utafiti, ambapo kwa kipindi cha muda mfupi alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa mjini Andalusia. Kufuatia kukosekana amani na usalama katika mji wa (Corduba, Qurtuba), Ibn Abdul Birr alilazimika kuhamia mji mwingine wa Daynah ambao kipindi hicho ulikuwa moja ya vituo muhimu vya elimu vya Andalusia, ambapo huko alifanikiwa kuandaa athari zake. Miongoni mwa athari za msomi huyu mashuhuri ni kitabu kiitwacho "Istiiab" ambacho kinahusu maisha ya masahaba wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw).
Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita, alizaliwa Edwin Hubble, mtaalamu wa elimu ya nyota wa Kimarekani. Awali alijiunga na chuo kikuu kusomea sheria kwa pendekezo la baba yake, hata hivyo baada ya kuhitimu alipendelea sana kusomea masuala ya nyota. Hivyo akaamua kusomea taaluma hiyo. Katika harakati hiyo Edwin Hubble aliufanyia utafiti mkubwa mrundikano mkubwa wa mawingu na pia vumbi na gesi angani. Kadhalika alithibitisha kupishana sayari nje ya mfumo wa Milky Way, kama ambavyo pia aliamini nadharia ya kupanuka kwa dunia. Edwin Hubble alifariki dunia mwaka 1953 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita alifariki dunia mwandishi mashuhuri wa Kirusi, Leo Tolstoy. Mwandishi huyo alizaliwa mwaka 1828 na aliondokewa na baba na mama yake akiwa bado mdogo. Alifanya safari za kitalii na uchunguzi katika jamii nyingi za Ulaya na mambo aliyoyashuhudia katika safari hizo yalimfanya achukie ustaarabu wa kimaada wa nchi za Magharibi. Tolstoy alilipa umuhimu mkubwa suala la kuwapa elimu na malezi watoto wadogo na alikuwa akijitahidi mno kusaidia matabaka ya watu maskini na wasiojiweza. Leo Tolstoy ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Kiyama", "Kipindi cha Utotoni" na riwaya ya "Vita na Amani".
Tarehe 20 Novemba miaka 102 iliyopita mapambano makubwa ya wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni wa Kiingereza yalishindwa. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kusambaratika utawala wa Kiothmania, serikali za Ufaransa na Uingereza ziligawana ardhi za utawala huo katika Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo Uingereza ilichukua Iraq na kukabiliwa na mapambano makali ya wananchi tangu hapo mwanzoni. Mapambano hayo yaliongozwa na wanazuoni wa Kiislamu waliotoa wito wa kufukuzwa wakoloni wa Kiingereza na kuundwa serikali huru itakayozingatia sheria za Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, aliuawa shahidi Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar huko Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Mwingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni wa Kiingereza na kumuuwa kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina.
Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita majeshi ya Marekani na China yalipambana uso kwa uso kwa mara ya kwanza kabisa katika vita vya Korea. Mapigano hayo yalitokana na himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa Korea Kusini na uungaji mkono wa China na Urusi kwa Korea Kaskazini. Vita vya Korea vilisababisha hasara kubwa mno kwa pande zote mbili. Vita hivyo vilisimama kutokana na upatanishaji wa Umoja wa Mataifa na hadi sasa Korea Kaskazini na Kusini zimebakia nchi mbili zilizojitenga.
