Jumamosi, 26 Novemba, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1444 Hijria ambayo inasafidiana na tarehe 26 Novemba 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita, yaani mwaka 1211 Hijiria, alifariki dunia mshairi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Kadhim Tamimi Baghdadi, maarufu kwa jina la Uzri akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa msomi na mwanafasihi mkubwa na ameacha diwani ya mashairi. Miongoni mwa mashairi ya malenga huyu maarufu wa Kiislamu ni shairi maarufu la "Al Uzriya" ambalo linamsifu Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu na kubainisha misingi ya dini ya Uislamu. Shairi hilo lina zaidi ya beti 1000. ***
Katika siku kama ya leo miaka miaka 167 iliyopita, Adam Bernard Mickiewicz mshairi na mwandishi mkubwa wa Kipoland aliaga dunia huko Istanbul uliokuwa mji mkuu wa utawala wa Othmania. Alizaliwa mwaka 1798. Kama alivyokuwa baba yake, Mickiewicz naye alikuwa mtu aliyekuwa akipigania uhuru. Aliishi katika zama ambazo nchi yake ya Poland ilikuwa imegawanywa na madola ya Prussia, Russia na Austria na alikuwa akifanya jitihada ili nchi yake iungane tena na kuwa kitu kimoja. Ni kutokana na sababu hiyo ndiyo maana mwaka 1823 alibaidishiwa nchini Russia. Baada ya miaka 6, Adam Mickiewicz alikimbilia nchini Ufaransa na kuanza kufundisha fasihi ya lugha. ***
Miaka 135 iliyopita Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku na sigara ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fatuwa hiyo ilitolewa baada ya mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni. ***
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, jeshi la kujitolea la wananchi (Basiji) liliundwa kutokana na amri ya Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuundwa jeshi la watu milioni 20 nchini Iran. Taasisi hiyo ya wananchi kutoka matabaka mbalimbali ya kijamii, kwa kuwa na wapiganaji wenye imani, moyo wa kujitolea na ari ya kuchapakazi imekuwa na nafasi muhimu katika matukio mbalimbali ya Mapinduzi ya Kiislamu hasa kipindi chote cha vita vya kujihami kutakatifu vya taifa la Iran dhidi ya uvamizi wa Iraq. Jeshi la Basiji bado linashiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiutamaduni na kijeshi hapa nchini Iran. ***
Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Ustadh Mirkhani, mmoja wa waalimu hodari wa Sanaa ya hati na maandishi ya kuvutia wa Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali alijifunza Sanaa ya hati kwa walimu mahiri wa Iran katika fani hiyo. Kwa muda mfupi Mirkhani aliweza kufikia daraja ya ualimu katika Sanaa hiyo na kisha akaanza kufundisha. Ustadh Mirkhani alikuwa na kipaji maalumu katikak Sanaa ya hati huku akiwa stadi pia katika utunzi wa mashairi. ***