Leo ni Jumapili tarehe 27 Novemba 2022
Leo ni Jumapili tarehe Pili Jamadil Awwal 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 27 Novemba 2022.
Miaka 1053 iliyopita siku kama hii ya leo, alifariki dunia malenga wa Kiirani Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Alizaliwa mwaka 341 Hijria katika mji wa Marv, moja kati ya miji ya Iran ya zamani, ambao hivi sasa unapatikana katika ardhi za Turkmenestan. Malenga huyu aliishi katika zama za mwisho za utawala wa Kisaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Maghaznavi. Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi kukisifu kizazi cha Mtukufu Mtume Muhammad (saw) hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha tungo kadhaa za mashairi.
Tarehe 27 Novemba miaka 103 iliyopita iliainishwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya kumalizika vita hivyo na kutiwa saini mkataba wa amani wa Versailles kulisainiwa mikataba mingine kadhaa ya kuainisha mustakabali wa tawala za Austria na Hungary na utawala wa Othmania na nchi ya Bulgaria ambayo kila mmoja ulikuwa na masharti mazito na kutoa fidia nchi hizo kwa zile zilizopata ushindi. Kuainishwa kwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati katika mkutano wa Paris kulibadili kikamilifu ramani ya dunia.

Katika siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, mkutano wa siku 3 wa viongozi wa Marekani, Uingereza na Umoja wa Sovieti ulifanyika mjini Tehran katika hali ambayo, Iran wakati huo ilikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya nchi hizo. Mkutano wa Tehran ulifanyika baada ya Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia na kuzuka kambi mpya dhidi ya jeshi la Ujerumani. Walioshiriki katika mkutano huo walikuwa Rais Franklin Delano Roosevelt wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill na Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti.
Miaka 75 iliyopita, mnamo tarehe 21 Rabiuthani 1371 Hijria, Ayatullah Muhammad Nahavandi, alimu mkubwa wa zama hizo aliaga dunia. Ayatullah Muhammad Nahavandi mwana wa mwanazuoni na alimu mchamungu Ayatullah Mirza Abdurahim Nahavandi, alizaliwa katika mji mtukufu wa Najaf, nchini Iraq. Kama alivyokuwa baba yake, Ayatullah Muhammad Nahavandi alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa karne ya 14 hijria kutokana na alivyojaaliwa kukwea na kufikia daraja za juu za elimu na akhlaqi njema. Tafsiri kubwa ya Qur’ani aliyofasiri kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi iitwayo Nafahaatu-Rahman na kitabu cha Dhiyaaul-Abs’aar fi Mabaahithil-Akhyaar ni miongoni mwa athari muhimu zilizoachwa na mwanazuoni huyo.
Miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Eugene O’Neill mwandishi Kimarekani. Eugene O’Neill ambaye alikuwa mashuhuri pia katika uandishi wa tamthilia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 65. Alizaliwa mwaka 1888 na maisha yake yalitawaliwa na matukio mengi. Eugene O’Neill alikuwa na mapenzi makubwa na tamthilia na ndio maana akapewa jina la mtoto wa tamthilia. Mwaka 1936 Eugene O'Neill alitunukiwa tuzo ya Nobel. Baadhi ya vitabu vya mwandishi huyu ni Mfalme Jones, The First Man na Days Without Ends.