Jumamosi, 31 Disemba, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 7 Mfunguo Tisa Jamadu-Thani 1444 Hijria mwafaka na tarehe 31 Disemba 2022 Miladia.
Miaka 919 iliyopita katika siku kama ya leo, arifu mkubwa wa Kiislamu Ainul Qudhaat Hamedani mwenye lakabu ya Abul Fadhl, aliuawa shahidi kwa kunyongwa huko Hamedam. Alikuwa fakihi, mwanafasihi, msomi na malenga mahiri. Ainul Qudhaat alizaliwa mwaka 492 Hijria. Msomi huyo katu hakuwa akiogopa kubainisha itikadi yake. Ni kutokana na misimamo yake hiyo thabiti ambapo mwaka 525 Hijria alitiwa mbaroni na kufungwa huko Baghdad. Baada ya muda alihamishiwa Hamedan na kunyongwa kando na shule yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Tamhiidat na Haqaiqul Qur’an. ***
Katika siku kama ya leo miaka 84 iliyopita yaani tarehe 7 Jamadut-Thani mwaka 1360 Hijria, aliaga dunia Ayatullah Abu Abdullah Zanjani mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alimu huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 51 na kuzikwa mahala alipozaliwa yaani Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alijifunza elimu za fasihi, falsafa na itikadi akiwa kijana mdogo. Baadaye Ayatullah Zanjani alielekea Najaf Iraq kwa shabaha ya kujiendeleza zaidi kielimu. Historia ya Qur'ani, Historia ya Maisha ya Mtume Muhammad SAW na Adhama ya Hussein bin Ali ni baadhi tu ya vitabu vya Ayatullah Zanjani vyenye thamani kubwa. ***
Tarehe 31 Disemba mwaka 1994 yaani miaka 28 iliyopita, Idhaa ya Kiswahili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliasisiwa kwa shabaha ya kufikisha sauti na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wazungumzaji wa lugha hiyo. Matangazo ya Idhaa hii yalianza sambamba na sherehe ya kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran yanahusu masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika. Kwa sasa unaweza kuyasikiliza matangazo yetu kwa njia ya moja kwa moja na kupitia hifadhi ya matangazo wakati wowote. Unaweza pia kuyapata matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran kupitia simu ya mkononi bila ya kutoa malipo yoyote isipokuwa gharama zako za kawaida za Intaneti kupitia njia ya kupakua aplikesheni ya matangazo yetu ya IRIB World Service. ***

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita iliundwa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait kwa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha pamoja Shia na wafuasi wa Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) kote duniani, kujenga uhusiano baina yao, kunyanyua juu kiwango cha shule za kidini, kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza baina ya wafusi wa Ahlul Bait na madhehebu nyingine za Kiislamu na kadhalika. ***
Katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Rais Boris Yeltsin wa Russia aliondoka madarakani na nafasi yake ikachukuliwa na Vladimir Putin. Kipindi fulani Yeltsin alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti. Boris Yeltsin alichaguliwa kuwa Rais wa Russia Januari mwaka 1991 na alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti mwishoni mwa mwaka 1991, aliendelea kuwa Rais wa Russia akitumai kwamba, kwa kutumia misaada ya kifedha ya Magharibi angeweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi yake ya kiuchumi. Kinyume na matarajio yake, viongozi wa madola ya Magharibi hawakutekeleza ahadi zao, hali iliyopelekea siasa za Rais Boris Yeltsin kushindwa. Kushambuliwa kijeshi eneo lililotangaza kujitawala la Chechnia na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo na majeshi ya Russia, ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika kipindi cha utawala wa Boris Yeltsin nchini Russia.