Jan 05, 2023 22:50 UTC
  • Ijumaa tarehe 6 Januari 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 13 Jumadithani 1444 Hijria sawa na tarehe 6 Januari 2023.

Tarehe 13 Jumadithani mwaka 64 Hijria kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria, alifariki dunia Fatima bint Hizam al Amiriyya al Kilabiyya, maarufu kwa laqabu ya Ummul Banin, mke mwema na mcha Mungu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). 

Wanahistoria wamehitilafiana juu ya siku aliyozaliwa, baadhi wanasema alizaliwa mwaka wa 5 baada ya Hijra ya Mtume (saw). 

Imam Ali bin Abi Twalib alimuoa bibi huyu mwema baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahraa (as). 

Ummul Banin anatoka katika kizazi cha mashujaa wakubwa wanaopigiwa mfano baina ya Waarabu. Baada ya kuolewa, mtukufu huyo alimuomba Imam Ali ampe laqabu ambayo atakuwa akiitumia kumwitia badala ya jina lake la Fatima ambalo alichelea kwamba litakuwa likiwakumbusha wajukuu wa Mtume mama yao, yaani Fatimatu Zahraa (as). 

Aliwapenda sana Ahlul Bait wa Mtume na historia inahadithia jinsi alivyowatuma wanae wote wanne kwenda kuilinda familia ya Mtume hususan Imam Hussain katika ardhi ya Karbala. Watoto wote wanne wa Hadhrat Ummul Banin, wakitanguliwa na Abul Fadhl al Abbas, waliuawa shahidi wakiwa pamoja na kaka yao, Hussein katika medani ya Karbala. Ummul Banin alifariki dunia katika siku kama ya leo mjini Madina na kuzikwa katika makaburi ya Baqii.   

Siku kama ya leo miaka 1014 iliyopita alifariki dunia Ibn Haytham, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu katika mji wa Cairo. 

Ibn Haytham alizaliwa mwaka 354 Hijiria katika mji wa Basra kusini mwa Iraq. Alibobea katika elimu za fizikia, tiba, falsafa na nujumu. 

Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya hisabati, nujumu na tiba. 

Moja ya vitabu vyake muhimu ni al-Manadhir ambacho kimetafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na kinatumika katika elimu ya nujumu. 

Ibn Haytham

Siku kama ya leo 162 iliyopita ilianzishwa nchi ya Romania. Mpango wa kuasisiwa nchi ya Romania ulibuniwa tarehe 13 Disemba 1859 kwa kuunganishwa miji miwili midogo ya Moldavia na Wallachia. Miaka miwili baadaye majimbo na miji mingine ilijiunga na umoja huo na kuundwa nchi ya Romania.  *

Bendera ya Romania

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita alifariki dunia Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran.

Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran.

Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi.

Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi na kutokuwa na wizani. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".

Nima Yushij

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita kulitokea hamasa ya mashahidi wa Huweize iliyoongozwa na Shahidi Alamul Huda katika miezi ya mwanzoni mwa uvamizi wa Iraq dhidi ya ardhi ya Iran.

Mwezi Dei mwaka 1359 Hijria Shamsia na baada ya jeshi la Iran ya Kiislamu kuvishinda vikosi zaidi ya viwili vya jeshi la Iraq huko kusini mwa eneo la Susangerd, kundi moja la Jeshi la Sepah la Ahwaz huko kusini mwa Iran lilitumwa katika mji wa Huweize kwenda kuulinda mji huo mbele ya mashambulizi ya Iraq. Hata hivyo kutokana na kuchelewa kufika zana na hujuma kubwa ya Iraq, jeshi la Iran lililazimika kurudi nyuma.

Wakati huo zaidi ya wapiganaji mia moja wa Jeshi la Sepah, wapiganaji wa kujitolea na wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi waaminifu wa Imam Khomeini wakiongozwa na Sayyid Muhammad Hussein Alamul Huda walibakia katika mji huo wa Huweize wakipambana na adui na wakauawa shahidi.

Baadaye jeshi la Iraq liliuvunja kabisa mji wa Huweize na kuusawazisha na ardhi. Pamoja na hayo ushujaa wa vijana hao shupavu wa Iran waliosabilia roho zao kulinda ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu umebakia hai katika historia ya Iran.