Feb 04, 2023 02:14 UTC
  • Jumamosi, 4 Februari, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 13 Rajab 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 4 Februari 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1467 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba, Ali bin Abi Twalib AS, ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw). Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib. Katika kipindi chake cha utotoni, Ali bin Abi Talib alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu. Mwishoni mwa mwaka wa Pili Hijria, Imam Ali AS alimuoa Bibi Fatimatul Zahra binti ya Mtume Mtukufu SAW. Imam Ali AS alishiriki kwenye vita vyote bega kwa bega na Mtume Mtukufu SAW isipokuwa vita vya Tabuk, na alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge. ***

 

Leo tarehe 13 Rajab zinaanza siku zinazojulikana katika dini kuwa ni "Siku Nyeupe" au siku za ibada ya Itikafu ambazo ni siku za tarehe 13, 14 na 15 za mwezi huu wa Rajab. Katika siku hizi waumini wanashauriwa kufanya ibada ya itikafu ya kukaa na kubaki katika sehemu au mahala maalumu hususan misikitini na maeneo matakatifu kwa ajili ya ibada na kumdhukuru Mwenyezi Mungu SW. Watu wanaofanya itikafu hutakiwa kufunga Saumu siku tatu mfululizo wakiwa katika jitihada za kuondoka katika minyororo ya dunia hii finyu na kujikuribisha kwa Allah. Ibada ya itikafu imehimizwa sana na Mtume Muhammad (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake. ***

 

Miaka 1164 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 279 Hijria, alifariki dunia Abu Isa Tirmidhi, hafidh wa Qur'ani Tukufu na mpokezi mashuhuri wa Hadithi za Mtume (saw). Tirmidhi alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa miaka mingi kwa ajili ya kujipatia elimu ya dini na kukusanya Hadithi. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi hodari wa Imam Bukhari na kitabu chake maarufu zaidi Jamiu Tirmidhi. Kitabu hicho kinahesabiwa kuwa miongoni mwa marejeo muhimu ya Hadithi katika madhehebu ya Suni. ***

 

Siku kama hii ya leo miaka 335 iliyopita Pierre Marivaux mwandishi wa riwaya na michezo ya kuigiza wa Kifaransa alizaliwa huko Paris nchini Ufaransa. Pierre alianza kujishughulisha na kazi ya sanaa tangu akiwa kijana na kwa muda fulani alishiriki pia katika michezo ya kuigiza hadi pale alipoanza kuandika michezo hiyo. Marivaux alipata umashuhuri mkubwa kutokana na ukosoaji wake katika uandishi wa riwaya. Marivaux ameacha athari nyingi za kimaandishi zikiwemo riwaya na michezo ya kuigiza ambapo miongoni mwake tunaweza kuashiria zile alizozipa majina kama ya The Prudent na Equitable Father, The Triumph of Love na The Life of Marianne. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita kulifanyika mkutano uliojulikana kwa jina la Yalta katika peninsula ya Crimea huko kusini mwa Urusi ya zamani. Mkutano huo uliwakutanisha pamoja  viongozi wa nchi za Uingereza, Marekani na Shirikisho la Urusi ya zamani (Churchill, Roosevelt and Stalin). Mkutano huo ulifanyika baada ya kudhihiri dalili za kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Lengo hasa la mkutano wa Yalta lilikuwa kujadili hali ya kisiasa na kijeshi ya nchi zilizokuwa zikipigana vita hivyo, ikiwa ni pamoja na kuainisha hatima ya ardhi zilizokuwa chini ya madola waitifaki. ***

 

Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo nchi ya Sri Lanka ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Nchi hiyo iliyoko kusini mashariki mwa India ilivamiwa na wakoloni wa Kireno katikati mwa karne ya 16 na baadaye wakoloni wa Kiholanzi na tangu mwaka 1798 iliunganishwa rasmi na makoloni ya Uingereza. Mapambano ya kupigania uhuru wa Sri Lanka yalianza mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia. Mwaka 1931 Uingereza ililazimika kutoa haki ya kutoa maoni kwa wananchi wa Sri Lanka na kuasisi baraza la kutunga sheria na baraza la utekelezaji. Hata hivyo nchi hiyo ilikuwa bado haijapata uhuru kamili katika masuala ya kigeni. Kwa msingi huo mapambano ya wananchi yaliendelezwa hadi kisiwa hicho kilipopata uhuru kamili mwaka 1948. ***

 

 

Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita wakati mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah yalipokuwa yamefika kileleni, Waziri Mkuu wa utawala wa kifalme hapa nchini Shapour Bakhtiar alifanya jitihada za kuzima vuguvugu la wananchi bila ya mafanikio yoyote. Bakhtiar alisema katika mahojiano na vyombo vya habari kwamba, hatamruhusu Imam Khomeini kuunda serikali ya mpito. Wakati huo uasi wa kiraia, kukimbia wanajeshi na kujiunga na safu za wananchi katika miji mbalimbali ya Iran ikiwa ni pamoja na kujiuzulu wabunge, viongozi wa ngazi za juu serikali na kadhalika viliifanya serikali ipoteze udhibiti wa mambo ndani ya nchi. ***

 

Na siku kama ya leo miaka 7 iliyopita aliaga dunia Raghib Mustafa Ghalwash qarii na msomaji Qur'ani mahiri wa Kimisri. Ghalwash alizaliwa Julai 5 mwaka 1938 nchini Misri na kukulia katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na Qur'ani. Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa tayari amehifadhi Qur'ani nzima katika rika la ubalobaro na kuanza kusoma kitabu hicho katika hafali na majlisi mbalimbali akiwa na umri wa miaka 16. Sheikh Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa miongoni mwa wasomaji wa Qur'ani waliofanya safari nchini Iran baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa vilivyoanzisha na Iraq dhidi ya Iran. Qiraa na kisomo cha gwiji huyo wa Misri kilipendwa sana nchini Iran. Hatimaye Qarii huyo mashuhuri aliaga dunia alfajiri ya Alkhamisi tarehe 4 Februari mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 77 baada ya kuugua kwa muda mrefu. ***

 

Tags