Feb 10, 2023 02:24 UTC
  • Ijumaa, tarehe 10 Februari, 2023

Leo Ijumaa tarehe 19 Rajab mwaka 1444 Hijria sawa na 10 Februari 2023.

Siku kama ya leo miaka 1435 vilitokea vita vya Tabuk baina ya Waislamu na jeshi la Roma. Vita vya Tabuk ni miongoni mwa vita vya mwisho vya Mtume Muhammad (saw).

Sababu ya kutokea vita hivyo ni kwamba, msafara wa kibiashara wa Sham ulimtaarifu Mtume (saw) kwamba mfalme wa Roma ametayarisha jeshi na kulituma Madina. Kwa msingi huo Mtume Muhammad (saw) aliwaanuru Waislamu kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la mfalme wa Roma.

Waislamu wengi walijitayarisha kwa ajili ya vita hivyo licha ya masafa marefu, msimu wa joto kali, mashaka ya safari hiyo ngumu na kuwadia msimu wa mavuno. Hatimaye jeshi na wapiganaji elfu 30 la Waislamu liliwasili eneo la vita lakini halikukuta jeshi la mfalme wa Roma eneo hilo.

Japokuwa hakukutokea mapigano wakati huo, lakini tukio hilo lilidhihirisha nguvu ya Waislamu, utayarifu wao wa kukabiliana na majeshi vamizi na moyo wao wa kujitolea kwa ajili ya Allah.

Vita hivyo vya Tabuk pia vinajulikana kwa jina la "al Fadhiha" kwa maana ya mfedheheshaji kutokana na kwamba, vililifedhehesha kundi la wanafiki waliokataa kujiunga na msafara huo kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la Roma. 

Miaka 970 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Rajab mwaka 474 Hijria Qamaria Abul Walid Sulaiman bin Khalaf Maliki, faqihi maarufu wa karne ya Tano Hijria Qamaria aliaga dunia huko Andalusia ambayo leo inajulikana kama Uhispania.

Alikuwa hafidh na mfasiri wa Qur'ani Tukufu mbali na kubobea katika fasihi na mashairi. Abul Walid awali alifunza Fiqhi na taaluma ya Hadithi za Mtume SAW huko Andalusia na kisha akaendelea kufundisha huko Makka na Baghdad.

Baadhi ya vitabu mwanazuoni huyo ni, "Tafsirul Qur'an", "An-Nasikh Walmansukh" na Al-Isharah." 

Siku kama ya leo miaka 260 iliyopita ulitiwa saini mkataba baina ya Uingereza na Ufaransa katika mji wa Paris.

Wafaransa waliutaja mkataba huo kuwa mbaya sana. Hii ni kutokana na kuwa, baada ya miaka mingi ya vita na mivutano na Uingereza, Ufaransa ilikubali kufumbia macho madai yake yote na maslahi yake ya kikoloni huko India na Canada.

Sababu ya kutiwa saini mkataba huo ni kwamba, katika kipidi hicho Ufaransa ilikuwa imedhoofika kutokana na kujihusisha na vita mbalimbali barani Ulaya, na kwa upande wa kijeshi na kiuchumi haikuwa na ubavu wa kuendelea kupigana vita na Uingereza. 

Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita alifariki dunia Sophia Krukovsky mwanahisabati wa Russia.

Alizaliwa mwaka 1850 mjini Moscow. Licha ya kuwa alipendelea sana elimu ya hisabati, lakini kutokana na sababu za kibaguzi hakuweza kujiunga na chuo kikuu na ni kwa msingi huo ndio maana akaelekea nchini Ujerumani na kujifunza elimu ya hisabati na fizikia.

Pamoja na hayo Sophia Krukovsky alikabiliwa na matatizo mengi kabla ya kufanikiwa kujiunga na chuo kikuu. Kufuatia hali hiyo alilazimika kusoma elimu hiyo kwa mwalimu wa hisabati nje ya chuo kikuu. Mwaka 1874 Sophia Krukovsky alitunukiwa shahada ya juu ya Uzamivu (PhD) bila kuhudhuria chuoni.

Mwaka 1888 alitunukiwa zawadi yenye itibari katika chuo cha academia nchini Ufaransa. Kuanzia mwaka 1884 hadi mwaka 1891 alipofariki dunia alijishughulisha na kazi ya ufundishaji wa hisabati katika Chuo Kikuu cha Stockholm, Sweden.

Sophia Krukovsky

Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, tawala za waitifaki na zile zilizokuwa zikihasimiana katika Vita vya Pili vya Dunia zilisaini makubaliano ya amani.

Katika siku hiyo, Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa zilisaini makubaliano ya amani na nchi zilizoshindwa katika vita hivyo yaani Italia, Finland, Poland, Hungary, Romania na Bulgaria, na kwa utaratibu huo nchi sita hizo kwa mara nyingine tena zikajipatia uhuru. 

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita yaani tarehe 10 Februari mwaka 1950, Joseph Mc Carthy Seneta wa chama cha Republican nchini Marekani aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo akiwatuhumu kuunga mkono ukomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani.

Hatua hiyo ilipelekea kuanza kwa kile kilichojulikana kama "Mc Carthisim" huko nchini Marekani, ambapo kwa mujibu wake wanafikra, wataalamu na viongozi mbalimbali wa Marekani walifuatiliwa na kusakwa baada ya kutuhumiwa kuwa na mitazamo na fikra za Kikomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani.

Kamisheni ya Mc Carthisim ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa, iliwafuta kazi karibu watumishi wa serikali wapatao 2000 huku idadi kubwa ya wataalamu na wasomi wakiswekwa jela kwa tuhuma zisizokuwa na msingi.

Joseph Mc Carthy

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita majenerali wa utawala wa Shah waliongeza muda wa serikali ya kijeshi katika mji wa Tehran.

Majenerali hao walichukua hatua hiyo ili kuwazuia wananchi kuwaunga mkono na kuwasadia wanajeshi wa kikosi cha anga ambao walikuwa wakishambuliwa na kikosi cha gadi ya Shah, na kwa njia hiyo waweze kumtia mbaroni Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu pamoja na shakhsiya wengine muhimu waliokuwa katika harakati za Mapinduzi au kuwauwa.

Hata hivyo Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuona mbali na kusoma vyema alama za nyakati, aliwatolea mwito wananchi kupuuza kizuizi hicho kilichowekwa na majenerali wa Shah cha kuongeza muda wa serikali ya kijeshi au sheria za kutotoka nje.

Wananchi wanamapinduzi wa Iran pia waliitikia agizo hilo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu na kumininika katika mitaa mbalimbali na kueneza mapambano yao katika vituo vingine vya kijeshi vya utawala wa kidikteta wa Shah katika mji wa Tehran na miji mingineo.  *

 

Tags