Jun 14, 2023 02:37 UTC
  • Jumatano, tarehe 14 Juni, 2023

Leo ni Jumatano tarehe 25 Dhilqaada 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 14 Juni mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita Nabii Muhammad (saw) aliondoka Madina akiwa na masahaba na Waislamu zaidi ya laki moja na kuelekea Makka kwa ajili ya kutufu nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba.

Tangu alipohamia Madina Mtume (saw) alielekea Makka mara tatu kutufu al Kaaba lakini alifanikiwa mara mbili tu kutekeleza ibada ya Hija. Katika safari yake ya mwisho ya Hija, Mtukufu huyo aliwafunza Waislamu namna ya kutekeleza ibada ya Hija kwa njia sahihi. Baada ya kukamilisha ibada hiyo, Mtume Muhammad (saw) alirejea Madina na alipofika katika eneo la Ghadir Khum aliwakusanya masahaba zake, na kwa amri ya Mola wake alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib kuwa Khalifa na Kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake. Hiyo ilikuwa safari ya mwisho ya Hija ya Mtume ambayo ni maarufu kwa jina la Hajjatul Widaa. Miezi kadhaa baada ya safari hiyo Mtume Muhammad (saw) aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake.

Katika siku kama ya leo miaka 287 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa kwa jina la Charles Augustin de Coulomb.

Msomi huyo alianza kufundisha masomo katika nyanja za umeme na sumaku baada ya kuhitimu masomo yake na kuandika vitabu vingi katika uwanja huo. Mbali na kufundisha, mwanafizikia Augustin de Coulomb aliendelea pia kufanya utafiti na hatimaye akafanikiwa kubuni kanuni katika sayansi ya fizikia iliyojulikana kwa jina lake. De Coulomb aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70. 

Charles Augustin de Coulomb

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Kamanda Muhammad Ali Pasha waliishambulia Sudan na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Wakati huo huo Waingereza pia walilishambulia eneo la kusini mwa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Hata hivyo wananchi wa Sudan wakiongozwa na Mahdi al Sudani mwaka 1881 walianzisha harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Misri na Uingereza na mwaka 1885 wakafanikiwa kutoa pigo kubwa kwa vikosi vamizi vya Misri na Uingereza na hivyo kuyakomboa maeneo hayo.  ***

Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita wanajeshi wa Ufaransa waliwasili katika pwani ya Algeria huko kaskazini mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa oparesheni za kijeshi za Ufaransa zilizokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria. Hata hivyo uvamizi huo wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria ulikabiliwa na mapambano makubwa ya wananchi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Mapambano hayo ya kupigania ukombozi ya wananchi wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa yalipamba moto baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hatimaye mwaka 1962 Rais wa wakati huo wa Ufaransa alilazimika kuipatia Algeria uhuru kamili kufuatia mashinikizo ya mapambano ya wananchi wa Algeria na upinzani wa fikra za waliowengi ndani ya Ufaransa kwenyewe na kimataifa. 

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita mto mrefu na mkubwa zaidi wa Asia wa Yangtze Kiang ulivunja kingo zake na kusababisha mafuriko ya kutisha. Mvua kali za msimu zilizonyesha zilisababisha mawimbi na mafuriko makubwa yaliyovunja kingo na mabwawa yote ya kandokando ya mto huo. Maji hayo yaligubika ardhi ya majimbo 8 ya China. Inasemekana kuwa tukio hilo kubwa liliathiri karibu watu milioni 50 wakiwemo waliopoteza maisha, kupoteza makazi, uharibifu wa mashamba, wale waliofariki dunia kutokana na maradhi ya aina mbalimbali na kadhalika. 

Mto wa Yangtze Kiang

Tarehe 24 Khordad miaka 42 iliyopita wawakilishi 120 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) waliwasilisha muswada wa kutokuwa na imani na Bani Sadr aliyekuwa rais wa wakati huo wa Iran. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kusambaratika mapambano ya wananchi dhidi ya wavamizi wa chama cha Baath kutoka Iraq katika hujuma iliyofanywa dhidi ya ardhi ya Iran kutokana na kukosa misaada ya dharura kutoka kwa Bani Sadr aliyekuwa Kamanda na Amri jeshi Mkuu, na vilevile hitilafu zilizojitokeza baina ya Rais wa nchi na mihimili mingine miwili ya dola.   

Bani Sadr

Na siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, alifariki dunia Jorge Luis Borges, mwandishi mkubwa wa Amerika ya Latini. Luis alizaliwa mwaka 1899 Miladia nchini Argentina na kutokana na kutalii sana athari za wasomi wakubwa kama vile Edgar Allan Poe, Charles Dickens na Cervantes akafanikiwa kuinukia na kuwa hodari katika uwanja huo. Mwishoni mwa masomo yake, Jorge Luis Borges akaanza shughuli ya uandishi na taratibu akaanza kuandika kisa mashuhuri cha Amerika ya Latini. Hata hivyo kutokana na upofu wake, hakuweza kumaliza kuandika kisa hicho. Luis ameacha athari mbalimbali za vitabu ambavyo vinapatikana katika maktaba mbalimbali za dunia.

Jorge Luis Borges

 

Tags