Jul 01, 2023 05:55 UTC
  • Jumamosi, Mosi Julai, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 12 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1444 Hijria sawa na tarehe Mosi Julai 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, nchi ya Canada ilijitangazia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Canada iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na kuanzia wakati huo kwa zaidi ya karne mbili, Uingereza na Ufaransa zilikuwa zikishindana katika ardhi ya nchi hiyo kwa lengo la kupanua udhibiti wao. Ushindani huo ulipelekea kujiri vita kati ya mataifa hayo ya kikoloni ambapo mwaka 1689 vita hivyo vilidumu kwa karibu miaka 75 vilimalizika kwa kushindwa Ufaransa. Kuanzia mwanzoni mwa karne ya 19 taratibu zilianza harakati za kupigania uhuru wa Canada ambazo zilizaa matunda mwaka 1867 katika siku kama ya leo. ***

Bendera ya Canada

 

Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo, sehemu mbili za Somalia ya Uingereza na ya Italia ziliungana na kuunda nchi moja ya Somalia yenye kujitawala. Karne kadhaa nyuma, Somalia iliwahi kujitawala kwa kipindi kifupi. Mwaka 1884 Uingereza iliiweka katika himaya yake sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Miaka mitano baadaye Italia nayo ikakoloni baadhi ya sehemu za Somalia. Harakati za mapambano za Muhammad Abdullah Hassan dhidi ya Waingereza kuanzia mwaka 1901 hadi 1920 hazikuzaa matunda. Mwaka 1950 Umoja wa Mataifa uliitaka Italia iandae mazingira ya kujitawala na kuwa huru nchi ya Somalia. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, nchi ndogo ya Burundi ilijitangazia uhuru wake. Kuanzia mwaka 1899 hadi 1917 Burundi pamoja na Rwanda ilikuwa sehemu ya makoloni ya Mjerumani huko Afrika Mashariki. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kushindwa Ujerumani katika vita hivyo, Umoja wa Mataifa uliikabidhi Ubelgiji ardhi ya Burundi. Mwaka 1962 Burundi ilipata uhuru ikiwa na mfumo wa utawala wa kifalme. Hata hivyo miaka minne baadaye wapigania jamhuri walimuondoa madarakani mfalme na kuanzisha mfumo wa serikali ya jamhuri. ***

Bendera ya Burundi

 

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, Rwanda ilipata uhuru. Rwanda ina historia inayofanana na jirani yake wa kusini yaani Burundi ambapo kabla ya nchi hizo kujitangazia uhuru zilikuwa zikikoloniwa na Ubelgiji. Baada ya mapambano mtawalia ya wapigania uhuru wa Rwanda, hatimaye mnamo mwaka 1962, nchi hiyo ilipata uhuru na kabila kubwa la Wahutu likashika hatamu za uongozi wa nchi. Mwaka 1973, Meja-Jenerali Juvenal Habyarimana alichukua madarakani baada ya kufanya mapinduzi yasiyo na umwagaji damu. Hata hivyo mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari ambapo zaidi ya watu laki 8 waliuawa wengi wao wakiwa ni wa kabila la Tutsi. ***

Bendera ya Rwanda