Jul 15, 2023 23:21 UTC
  • Leo Katika Historia

Leo ni Jumapili Mwezi 27 Mfunguo Tatu Dhul-Hijjah 1444 Hijria sawa na tarehe 16 Julai 2023 Miladia.

Miaka 753 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 27 Dhul-Hijjah mwaka 691 Hijria, aliaga dunia Sheikh Muslihuddin Saadi Shirazi, mshairi mbobezi na malenga mtajika wa mashairi na nathari za lugha ya Kifarsi. Baada ya kuhitimu masomo ya utangulizi ya elimu za fasihi na dini katika mji alikozaliwa wa Shiraz, Saadi alisafiri kuelekea mji wa Baghdad akiwa bado kijana. Katika madrasa ya Nidhamiyah ya mji huo alijifunza elimu maarufu za zama hizo; na baada ya kuhitimu alisafiri kuelekea ardhi za Sham, Falast'in, Hijaz, Roma na nchi zingine. Wakati wa safari zake hizo, Saadi alipata kujuana na watu wa jamii tofauti; na kutokana na aliyoyasikia na aliyojionea, alitumia ustadi wake wa ushairi kusanifu mashairi ya kuvutia. Hatimaye alirudi mji alikozaliwa wa Shiraz alikoendelea kusanifu na kuanza kualifu vitabu vya athari zake kwa kutumia uzoefu na tajiriba ya miaka 30 ya kusafiri na kutalii miji na nchi mbalimbali pamoja na kujuana na watu wa aina tofauti. Mnamo mwaka 655 Saadi alihitimisha uandishi wa kitabu chake adhimu cha masuala ya tabia na malezi cha Bustan, ambacho mashairi yake aliyatunga akiwa safarini. Ndani ya kitabu hicho, yanazungumziwa masuala ya haki na uadilifu, kufanya ihsani, unyenyekevu, upendo, kukinai, malezi, toba n.k. Athari nyingine maarufu ya malenga huyo mtajika wa Iran ni Golestan. Mahali alikozikwa Saadi katika mji wa Shiraz, kila siku hupokea wapenzi na maashiki wa lugha na fasihi ya Kifarsi kutoka kila pembe ya dunia.

Saadi Shirazi

Katika siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, yaani Julai 16 1890, maradhi ya Utetemekaji yaani Parkinson pamoja na sababu zake viligunduliwa na tabibu Muingereza aitwaye James Parkinson. Na hii ndio sababu ya ugonjwa huo kutambuliwa kwa jina la tabibu huyo. Dalili za maradhi ya utetemekaji ni mtetemo mkali na wa kudumu wa mkono, ulimi na kichwa na kushindwa mtu kuwa sawa anapotembea hususan katika umri wa uzee. Sababu kuu ya ugonjwa wa utetemekaji ni mvurugiko unatokea kwenye ubongo; na hadi sasa dawa mjarabu ya kuutibu bado haijapatikana.

Parkinson

Miaka 71 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia ya Kiirani, yaani tarehe 25 Tir mwaka 1331 Dakta Mosaddegh alijiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu. Dakta Mohammad Mosaddeqh alikwenda kukutana na Mfalme Mohammad Reza Shah Pahlavi tarehe 25 Tir 1331 baada ya kuchgauliwa tena na bunge na kuwasilisha kwake orodha ya majina ya mawaziri wake. Katika mkutano huo Mosaddeqh alimwomba Shah amkabidhi yeye pia nafasi ya waziri wa ulinzi kwa madai kwamba wanajeshi hawayapi umuhimu maagizo anayowapa na wanakwamisha mambo. Na kwa hali hiyo, serikali haiwezi kuendelea na kazi zake. Shah alikataa ombi hilo la waziri mkuu. Mosaddeqh alirudi nyumbani kwake na kumwandikia barua Shah ya kujiuzulu. Shah alimteua Qawam Saltanah kuwa waziri mkuu, na siku chache tu baada ya kushika wadhifa huo, Qawam alitoa tangazo kwamba serikali itapambana vikali na wapinzani wake. Hatua za Qawam, ambazo ziliungwa mkono kwa kila hali na Shah ziliwafanya wananchi na maulamaa waamue kusimama dhidi yake. Hatimaye matukio hayo yakawa sababu ya kujitokeza wananchi katika maandamano makubwa ya Tir 30 1331 yaliyopelekea Mosaddeqh kurudi tena madarakani.

Mohammad Mosaddeqh

Miaka 15 iliyopita, tarehe 16 Julai 2008 Hizbullah ya Lebanon ilipata mafanikio mengine, kwa kukabidhi miili ya askari wawili wa utawala wa Kizayuni wa Israel mkabala wa kuwakomboa mateka watano Walebanon na viwiliwili karibu 500 vya Mashahidi wa nchi hiyo kutoka mikononi mwa utawala wa Kizayuni. Mabadilishano ya mateka na miili hiyo yalifanyika kufuatia mazungumzo ya muda mrefu baina ya pande mbili kupitia Ujerumani. Kinachotoa mguso katika zoezi hilo la mabadilishano ni kwamba hadi dakika ya mwisho, vyombo vya intelijensia na ujasusi vya wazayuni havikuwa vikijua kama askari wao wawili walikuwa wameuawa tokea yalipotokea mapigano baina yao na wanamapambano wa Hizbullah na si kwamba wako hai wamekamatwa mateka. Miongoni mwa mateka Walebanon walioachiwa huru walikuwemo pia wanachama wa makundi mengine ya wanamapambano, muhimu zaidi ni Sameer Qant'ar, ambaye alisota kwenye jela za utawala wa Kizayuni kwa takriban miaka 30. Mabadilishano hayo ya mateka yalitambulika kama ushindi mwingine kwa harakati ya muqawama ya Hizbullah dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, na kwa sababu hiyo sherehe za kitaifa zilifanyika nchini Lebanon.

Sameer Qant'ar

Na miaka minane iliyopita katika siku kama hii ya leo, mnamo Juni 16, 2015 Sayyid Mutawalli Abdulaal, msomaji Qur'ani maarufu wa Misri alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1947 katika kijiji kilichoko kwenye mkoa wa Ash-Sharqiyyah nchini Misri. Baba yake alikuwa akiitwa Mutawalli na Sayyid ni jina lake yeye, ambalo alipewa na mama yake kwa sababu ya kumpa heshima maalumu Sheikh Sayyid Ahmad al-Badawy. Sayyid Mutawalli alianza kujifunza Qur'ani tangu akiwa mdogo, na alipofika umri wa miaka 12 alikuwa ameshahifadhi Qur'ani yote. Nukta moja inayompambanua Sayyid Mutawalli Abdulaal na maqaarii wengine wengi wa Qur'ani ni mtindo mpya wa usomaji ambao aliuanzisha akiwa na umri wa miaka 13 tu. Msomaji huyo mtajika aliwahi kuizuru Iran mara kadhaa na akatamka yafuatayo kuhusu Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wa Iran: "Sijawahi kuona popote duniani watu kama wa taifa la Iran; na ni watu wa aina yake kwa kuwa na mapenzi makubwa mno ya Qur'ani na ya kukipa umuhimu Kitabu hiki cha mbinguni kulinganisha na mataifa mengi. Hili nimejionea mimi mwenyewe kwa macho yangu; na ninaweza kusema kuwa katika nchi nilizotembelea, na bila ya kutia chumvi, katika hili nyinyi ni taifa ambalo hakuna mfano wenu". Hatimaye katika siku kama ya leo, qaarii na bingwa huyu wa usomaji Qur'ani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 68 na kuzikwa katika kijiji alikozaliwa mkoani Ash-Sharqiyyah nchini Misri.../

Sayyid Abdulaal Mutawalli