Uzayuni wa Kikristo na Israel
(last modified Sat, 27 Jan 2024 09:00:32 GMT )
Jan 27, 2024 09:00 UTC
  • Uzayuni wa Kikristo na Israel

Makala yetu ya wiki hii inahusu nafasi ya Uzayuni wa Kikristo katika kuendeleza vita vya Gaza na kuzuia amani.

Uzayuni wa Kikristo (Christian Zionism) ni mojawapo ya lobi muhimu za Mayahudi nchini Marekani, ambayo inaathiri maamuzi ya Ikulu ya Rais wa nchi hiyo, White House na utawala wa Israel kuhusu Wapalestina. Katika uchunguzi wa nyuma wa pazia wa waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza, kuna vielelezo madhubuti vya nafasi kubwa ya harakati yenye nguvu ya Wazayuni Wakristo wa Marekani, kiasi kwamba baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, maafa ya sasa ya kuwalazimisha Wapalestina kuyahama makazi yao, na vilevile mauaji yanayoendelea dhidi ya taifa hilo, vinafadhiliwa kwa mamilioni ya dola yanayotolewa kila mwaka na Wazayuni wa Kikristo kwa serikali ya Israel.

Katika miezi michache iliyopita, ulimwengu umeshuhudia kuendelea kwa mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, uvamizi wa kikatili wa kijeshi na kulazimishwa kuyahama makazi yao na utawala dhalimu wa Israel. Kwa sasa duniani kote kunasikika wito wa kuwepo mshikamano na watu wanaodhulumiwa wa Palestina na jibu la kimataifa kwa vitendo vya kinyama na kikatili vya serikali ya Israel. Wakati huo huo, Wazayuni wa Kikristo wanatoa wito kwa Marekani kuzidisha himaya na misaada yake isiyo na masharti kwa mpango wa Israel wa kuwatimua Wapalestina kutoka (Baitul Muqaddas) Jerusalem na kuwashambulia kwa mabomu raia wa Palestina huko Gaza. Wakati huo huo inaonekana kwamba, nafasi na mchango mkubwa wa harakati yenye nguvu ya Uzayuni wa Kikristo, katika zama za sasa na katika historia ndefu na ya umwagaji damu ya ukoloni wa Israel huko Palestina, inafifizwa na kutoweka katika simulizi nyingi. 

Mauaji ya kimbari Gaza 

Viongozi Wazayuni wa Kikristo daima wanayaarifisha mapambano ya ukombozi ya wa Palestina kama nembo ya chuki dhidi ya Wayahudi. Hivi majuzi tu, John Hagee, rais na mwanzilishi wa Christian United for Israel (CUFI), ambalo ni kundi kubwa zaidi la ushawishi linaloiunga mkono Israel nchini Marekani, alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X akisema kwamba Jerusalem na Israel ni mali ya Wayahudi. Katika ujumbe huo, John Hagee aliwahimiza Wakristo "kusimama dhidi ya uovu" na kuonyesha "upendo na himaya yao isiyo na mpaka kwa Israel."

Hapa linajitokeza swali kwamba, Uzayuni wa Kikristo, ambao ni kundi la ushawishi na lenye nguvu kubwa zaidi nchini Marekani katika kuiunga mkono Israel, una aidiolojia na mtazamo wa namna gani kuhusu ulimwengu?

Wanaharakati wa kundi hili la Wakristo Wazayuni wanaamini kwamba, Wayahudi watachukua udhibiti wa eti nchi ya Biblia ya Israel na kusababisha mwisho wa dunia. Kwa mujibu wa itikadi ya kundi hili lenye msimamo mkali, wakati Wakristo watakapookolewa, wasio Wakristo, wakiwemo Waislamu, wataangamizwa. Itikadi na mtazamo huu kuhusu ulimwengu, ambao una mizizi katika Uprotestanti wa karne ya 16 huko Ulaya, unaakisi mazingira ya ukoloni ya kipindi hicho.

Mtazamo huu unafafanua Uzayuni wa Kikristo (Christian Zionism) kama vuguvugu la kisiasa na kama sehemu ya harakati yenye misimamo mikali "fundamentalist movement". Mtazamo huu ulipata nguvu na kuimarishwa wakati watu kama Lord Shaftesbury, John Nelson Derby na William Blackstone, walipotabiri mwisho wa dunia na kuhubiri wazo la nchi ya Kiyahudi huko Palestina. Arthur James Balfour, Muingereza aliyetoa Azimio la Balfour (lililotoa ahadi ya kuanzishwa nchi ya Kiyahudi huko Palestina), pia alikuwa Mzayuni Mkristo. Vilevile Rais Woodrow Wilson wa Marekani alitia saini tamko hilo la Balfour kwa kushajiishwa na Jaji wa Mahakama ya Juu aliyekuwa Mzayuni wa Kiyahudi, Louis Dembitz.

Inatupasa kusema hapa kuwa, Uzayuni wa Kiyahudi ni toleo la juu na jipya zaidi la Uzayuni wa Kikristo. Wazayuni wengi wa Kiyahudi barani Ulaya wanakubaliana katika suala la kuanzisha dola ya Kiyahudi na kuwaunganisha Wazayuni Wakristo. Kwa hakika, ni Wazayuni wa Kikristo ndio waliojitwika jukumu la kuanzisha nguvu ya kibeberu na kijeshi kwa ajili ya kuikalia kwa mabavu Palestina baada ya kuanguka kwa Dola ya Othmania (Ottoman Empire). Jumuiya ya Mataifa ambayo baadaye ilibadilika na kuwa Umoja wa Mataifa, iliyoongozwa na mataifa yenye nguvu ya Wakristo wa Magharibi, hatimaye iliimega ardhi ya Palestina. Wazayuni wa Kikristo waliliona suala la kuhamisha Wayahudi kutoka Ulaya hadi Palestina kuwa ndio suluhisho linalofaa kwa "tatizo la Wayahudi". Kwa mujibu wa uamuzi huo, dola la Kiyahudi liliundwa kama mwakilishi wa maslahi ya kibeberu ya Magharibi katika eneo la kimkakati la Magharibi mwa Asia.

Wazayuni wengi wa Kikristo wanakuona kuanzishwa dola la Israel huko Palestina mwaka 1948, ambako kuliandamana na kufukuzwa Wapalestina wapatao 750,000, kuwa ni kutimia kwa utabiri wa Biblia. Hatua ya Israel ya kuvamia na kukalia kwa mabavu maeneo ya Ukingo wa Magharibi, Gaza, na Miinuko ya Golan, iliyoanza mwaka 1967, inatafsiriwa kuwa ni ishara kwamba Mungu anaibariki Israel na inatayarisha njia ya kurudi Yesu Kristo. Vita vilivyofuatia, uvamizi, na hujuma vinaonekana kuwa vitendo vinavyotoa bishara ya Aheri Zamani na nyakati za mwisho wa dunia ambazo zitawafikisha Wakristo kwenye uokovu, na kuwaangamizwa wasio Wakristo. Kwa maneno mengine ni kuwa, Uzayuni wa Kikristo unakaribisha vita, hasa uvamizi wa Israel dhidi ya Wapalestina; Kwa sababu wengi wao huiona Israel kuwa na ukuu wa kiteleolojia ambao ni bora zaidi kimaadili kuliko mahali au watu wa maeneo mengine duniani. Wazayuni hawa wa Kikristo hudhani kwamba, wanawaunga mkono watu wateule katika Nchi ya Ahadi, na kwa mtazamo huu vita yoyote katika jitihada hizi za utakaso inatambuliwa kuwa "vita vya haki".   

Miinuko ya Golan 

Hii leo, inakadiriwa kwamba, idadi ya Wazayuni Wakristo inafikia kwa uchache makumi ya mamilioni ya watu, ambayo ni zaidi ya idadi ya Wayahudi wote duniani. Huko Marekani, Wazayuni wa Kikristo ndio kambi kubwa zaidi na mrengo wa kulia ya wapiga kura wanaoiunga mkono Israel. Shirika kubwa zaidi la Wazayuni wa Kikristo, (Christians United for Israel (CUFI), lina wanachama milioni 10, na linajumuisha wanachama 100,000 wa American Israel Public Relations Committee au IPAC kwa kifupi, (ambayo ni lobi maarufu zaidi ushawishi ya Israel nchini Marekani). Mmoja kati ya kila watu wazima wanne nchini Marekani anajitambulisha kuwa Mkristo wa Kievangelisti, na asilimia 80 ya Wakristo wa Kiinjilisti, au asilimia 20 ya wakazi wa Marekani, wanaamini kwamba kukusanywa kwa mamilioni ya Wayahudi katika ardhhi ya Palestina kunakofanywa na serikali ya Israel kunaonyesha kwamba, ujio wa pili wa Isa Masia hapa duniani, unaokaribia.

Wakati huo huo takwimu zinaonyesha kuwa, siasa na sera nyingi za Marekani dhidi ya Palestina zinapangwa na kusimamiwa na Wazayuni Wakristo. Kwa mfano, sera ya mambo ya nje ya Donald Trump kuhusu Israel iliweza kuvutia mkondo wa Wakristo wa Kievangelisti kwa kiasi kikubwa. Wazayuni Wakristo, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo na Makamu wa Rais Mike Pence, walishika nyadhifa za juu zaidi katika utawala wa Trump. Vilevile katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Trump, ulimwengu ulishuhudia mabadiliko makubwa ya mrengo wa kulia katika sera ya Marekani kuhusu Israel.

Kwa kuzingatia haya yote inaonekana kuwa, kupuuza taathira za Uzayuni wa Kikristo katika ukoloni wa Israel huko Palestina ni kupuuza harakati kuu na kubwa zaidi ya kimataifa inayouunga mkono utawala ghasibu na katili wa Israel. Harakati hii inafuatilia udhibiti kamili wa Wayahudi huko Palestina. Uzayuni wa Kikristo umeongoza sera za Magharibi kuhusu Palestina tangu kwa uchache wakati wa Azimio la Balfour mwaka 1917 na bado ni uti wa mgongo wa himaya na uungaji mkono wa kimataifa kwa uvamizi wa Wazayuni na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina. Suala hili linatambuliwa kuwa ni kikwazo kikubwa cha kitheolojia cha kukomeshwa vita kati ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Baada tu ya kuanza Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya binadamu huko Gaza, kundi la waungaji mkono kwa Mayahudi wa Israel katika harakati ya Uzayuni wa Kikristo (Waevangelisti) lilizidisha uungaji mkono wake kwa utawala huo unaoendelea kuua watoto wadogo. Katika wiki mbili tu za kwanza baada ya kuanza kwa vita kati ya Palestina na Israel mnamo Oktoba 7, 2023, kundi la lobi na ushawishi la kievangelisti lilitoa msaada wa dola milioni 5 kwa Israel.

Kimbunga cha Al Aqsa 

"Waevangelisti" pia wamekuwa wakilishawishi Bunge la Marekani kwa nguvu zao zote kwa ajili ya maslahi ya Israeli kwa miaka mingi sasa. Kundi hili lenye itikadi kali katika vuguvugu la Wazayuni Wakristo, linafanya maandamano ya kuunga mkono Israel na kuzidisha ushawishi wake katika maamuzi yanayoipendelea Tel Aviv kwa kuwaingiza watu wake katika muundo wa madaraka na uongozi nchini Marekani. Kundi hili, linatumia makanisa yake mengi, kucheza na kupindua maoni ya umma na vilevile kuchangisha pesa ili kuendeleza sera za kujitanua za Israel katika ardhi ya Palestina.

Kuanzishwa kwa Israel mwaka 1948, kutekwa kwa Baitul Muqaddas (Jerusalem) na jeshi la Israel katika vita vya siku sita mwaka 1967, na kuhamishiwa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem kutoka Tel Aviv ni miongoni mwa bishara za Akheri Zamani (apocalyptic) zilizoko katika Biblia ya Waevangelisti, ambazo zote zimeunufaisha utawala wa Kizayuni katika kanda ya Magharibi mwa Asia. Bishara zingine mbili za madhehebu hii ni kujengwa upya eti eneo takatifu la Wayahudi kwenye Mlima wa Hekalu (ambako kunalazimu kuharibiwa Msikiti wa Al-Aqsa) na udhibiti wa baadaye wa na Israel juu ya Palestina nzima.

Pamoja na hayo yote, ushahidi unaonyesha kuwa, Waevangelisti vijana hawavutiwi sana na itikadi zinazohusiana na nafasi ya Israel katika teolojia ya apocalyptic ikilinganishwa na wazazi au babu zao. Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Barna Group katika Chuo Kikuu cha North Carolina uligundua kwamba, Waevangelisti vijana hawaiungi mkono Israel kama ilivyo kwa Waevangelisti wa makamo. Uchunguzi huo unaonyesha mabadiliko makubwa katika mitazamo yao kati ya 2018 na 2021, huku uungaji mkono kwa Israeli miongoni mwa Waevangelisti vijana ukishuka kutoka asilimia 75 hadi 34.

Tukilinganisha mwaka wa 2015 na 2018, tunaona kuwa mwaka wa 2015, asilimia 40 ya Waevangelisti vijana waliafiki msaada wa Marekani kwa Israel, na idadi hii ilifikia asilimia 21 mwaka 2018. Mwaka 2015, ni asilimia tatu tu kati yao walioipendelea Palestina, wakati mwaka 2018 asilimia hiyo ilifikia asilimia 18, na tofauti ya asilimia kati ya wafuasi wa pande hizo mbili pia ilipungua kutoka asilimia 37 hadi asilimia tatu.