Feb 14, 2024 17:33 UTC
  • Simulizi ya Hamas kuhusu Kimbunga cha Al Aqsa

Hamjambo na karibuni katika Kipindi chetu wiki hii ambacho kitaangazia simulizi za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kuhusu kwa nini Oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa ilitekelezwa.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) tarehe 4 mwezi huu wa Februari  ilitoa taarifa na kueleza sababu ya kutekelezwa Oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Hamas ilitangaza katika taarifa hiyo kwamba mapambano ya taifa la Palestina dhidi ya wavamizi na ukoloni hayakuanza tarehe 7 Oktoba 2023, bali yalianza miaka 105 iliyopita. Taifa la Palestina lilikuwa chini ya ukoloni wa Uingereza kwa miaka  30,  na kwa miaka 75  sasa ardhi yake inakaliwa kwa mabavu na  Wazayuni. Mwaka 1918 taifa la Palestina lilikuwa likimiliki asilimia 98.5 ya ardhi za Palestina na asilimia 92 ya wakazi wa ardhi hiyo walikuwa Wapalestina mkabala wa Wayahudi wachache, ambao aghalabu yao walikwenda katika ardhi hiyo  kupitia uhamiaji wa awali wa Wayahudi. Hadi kabla ya mwaka 1948, yaani kabla ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel, pamoja na kuwa mkoloni Muingereza alikuwa amefungua milango ya uhamiaji wa Wayahudi kuelekea ardhi ya Palestina na kujaribu kuwaandalia mazingira bora ili kuunda serikali yao, hata hivyo Wazayuni walidhibiti asilimia 6 tu ya ardhi ya Palestina na walikuwa asilimia 31.7 ya wakazi wa ardhi hiyo (licha ya wimbi lao kubwa la uhamiaji.) Tokea wakati huo hadi sasa Wapalestina, kwa miongo kadhaa sasa, wanaishi katika hali ya mateso, ukatili na mauaji yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwa ni pamoja na kunyimwa haki zao za msingi huku utawala huo ukitekeleza sera za kibaguzi dhidi ya raia hao. 

Uvamizi wa Israel huko Palestina tokea mwaka 1948 

Taarifa ya harakati ya Hamas imeongeza kuwa: Tangu miaka 17 iliyopita hadi sasa, Ukanda wa Gaza uko chini ya mzingiro mkali, na eneo hilo limekuwa jela kubwa zaidi isiyo na paa duniani. Ukanda wa Gaza pia umeathiriwa na vita vitano vya uharibifu; na mara zote Israel ndiyo iliyoanzisha vita. Vilevile tangu mwaka 2,000 hadi Septemba 2023 maghasibu wa Kizayuni wamewauwa shahidi Wapalestina 11,299 na kujeruhi 156,768, aghalabu yao wakiwa ni raia wa kawaida. 

Hamas imeeleza kuwa: Mwakilishi wa Israel katika Umoja wa Mataifa aliichana ripoti ya Baraza la Haki za Kibinadamu la UN mbele ya wawakilishi wa nchi mbalimbali duniani. Israel kivitendo imefutlia mbali uwezekano wa kuasisiwa nchi ya Palestina kwa hatua zake za mabavu na kupenda kujitanua za kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi, lengo likiwa ni kulifanya eneo hilo kuwa la Kiyahudi.  

Harakati ya Hamas imeendelea kwa kuhoji kwamba, je, taifa la Palestina lilitarajiwa kuendelea kusubiri hadi lini hatua za Umoja wa Mataifa na mashirika yake yasiyo na msaada kuhusiana na uvamizi na ukatili wa Israel?

Taarifa hiyo inaendelea kueleza kuwa: Operesheni ya kimbunga cha Al-Aqsa ilikuwa hatua ya lazima kwa ajili ya kukabiliana na njama zilizokuwa zimeratibiwa za kufutilia mbali kadhia ya Palestina. Kimbunga cha Al Aqsa kilitekelezwa ili kukabiliana na mipango ya Tel Aviv za kuzidhibiti ardhi zaidi za Palestina na Msikiti wa Al Aqsa. Oparesheni ya Kimbunga cha  Al-Aqsa ilikuwa hatua ya lazima na muhimu ya kukomesha mzingiro wa kikatili dhidi ya Ukanda wa Gaza na inatambuliwa kuwa harakati ya kujikomboa kutoka kwenye makucha ya maghasibu wa Kizayuni. 

Hamas imesisitiza kuwa: Oparesheni hiyo ni hatua ya kawaida kwa ajili ya kupigania ukombozi na kuwa huru Palestina, sawa kabisa na mataifa mengine, na pia kupigania haki ya kuianisha mustakbali wa taifa hilo. Kimbunga cha Al Aqsa ilikuwa hatua ya lazima kwa ajili ya kuasisi nchi huru ya Palestina, mji wake mkuu ukiwa Quds. Oparesheni hiyo ya Oktoba 7 mwaka jana ililenga maeneo na kambi za jeshi la Israel, ambapo zilifanyika jitihada za kuwakamata mateka askari jeshi wa adui kwa lengo la kuwakomboa mateka wa Kipalestina.  

Harakati ya muqawama ya Kiislamu ya Palestina (Hamas)

Taarifa ya Hamas imeendelea kueleza kuwa: Operesheni hiyo ilijikita katika kuwashambulia wanajeshi wa Israel eneo la Gaza na maeneo mbalimbali ya utawala wa Kizayuni katika vitongoji vya walowezi karibu na Ukanda wa Gaza. Hamas imesisitiza kuwa: Suala la kuepusha kuwashambulia  raia, hasa wanawake, watoto na wazee ni maagizo ya kidini na kimaadili yanayoheshimiwa na kutekelezwa na watoto wa Hamas. 

Imesema, Muqawama wa Kiislamu wa Palestina unafuata sheria na amri za dini ya Kiislamu, na tawi la kijeshi la harakati hiyo linawashambulia wanajeshi ghasibu na wale wote wanaoshika silaha dhidi ya taifa la Palestina. Kwa msingi huo, wanamuqawama wa Palestina wanajiepusha kuwashambulia raia licha ya kutokuwa na silaha makini na za kisasa. Harakati ya Hamas imesisitiza kuwa, raia wa Israel waliotekwa nyara Ukanda wa Gaza wameshughulikiwa vyema na kwa mwenendo mzuri. Tangu siku ya kwanza ya Oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa zimefanyika juhudi kubwa ili mateka hao waachiwe huru haraka iwezekanavyo.  

Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa: Propaganda za Wazayuni maghasibu kwamba Brigedi za  Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, ziliwashambulia raia wa Israel katika tukio la 7 Oktoba ni uongo na uzushi. 

Wanamuqawama wa Qassam kamwe hawakuwashambulia raia, bali aghalabu yao waliuliwa na polisi na jeshi la Israel. Madai kwamba vikosi vya wanamapambano wa Palestina viliwauwa watoto wachanga 40 yamekanushwa vikali na wanamapambano wa Palestina, kama ambavyo pia duru za Israel zimekadhibisha madai hayo. Hamas pia imetangaza kuwa: Mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza yameua raia wengi wa Israel ambao walitekwa nyara Oktoba 7 mwaka jana. Mashambulizi hayo ya utawala wa Kizayuni yanaonyesha kuwa maghasibu hawajali wala kuheshimu hata uhai wa mateka wao wenyewe na wako tayari kuwatoa kafara. Tarehe 7 Oktoba, baadhi ya walowezi wa Kizayuni waliokuwa na silaha walipigana na wanamapambano wa Palestina; ambapo utawala wa Kizayuni uliwasajili walowezi hao kama raia waliouawa. Uchunguzi usioegemea upande wowote utathibitisha simulizi ya harakati ya Hamas na kukanusha madai ya Israel. 

Wanamuqawama wa Izzudin Qassam 

Taarifa ya Hamas inaendelea kusema: Tunaziomba nchi mbalimbali ziunge mkono suala la kufanyika uchunguzi huru kuhusu jinai zilizofanywa huko Palestina. Wananchi wa Palestina wanaiomba Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) itume  haraka timu yake huko Palestina kwa ajili ya kufanya uchunguzi huru kuhusu jinai na ukiukwaji wote za sheria uliofayika. Hamas imeongeza kuwa, matukio ya tarehe 7 Oktoba yanapaswa kuchambuliwa katika upeo mpana; na mifano ya mapambano ya ukombozi katika historia ya sasa duniani inapaswa kukumbukwa. Nchi za Magharibi hazitaki kukubali kuwa chimbuko na chanzo cha  mgogoro  ni kuwepo Wazayuni maghasibu na kuporwa haki ya watu wa Palestina ya kuishi kwa uhuru na amani.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa: Harakati ya Hamas ni harakati halali ya kupigania ukombozi wa kitaifa, na kila taifa lina haki ya kujihami na kujilinda. Mapambano ya kukabiliana na wavamizi kwa kutumia njia yoyote, ikiwemo kujihami kwa silaha, yamehalalishwa na dini zote na sheria za kimataifa.   

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeongeza kufafanua kwamba: Tangu kuasisiwa utawala bandia wa "Israel", Marekani na washirika wake wa Kimagharibi wamekuwa wakiukingia kifua na kuuhami utawala huo kwa hali na mali ili uendelee kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na kukandamizwa watu wake. Hatua nyingine zilizofanywa na Wazayuni kwa himaya na msaada wa nchi za Magharibii ni pamoja na kunyakua ardhi zaidi za Wapalestina, kuyavunjia heshima maeneo matakatifu, kuziyahudisha ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, kusabisha hali ngumu na duni ya maisha kwa Wapalestina, na kufanya jitihada za kuwafurusha raia wa Palestina na kuwalazimisha kuhama ardhi na nchi yao.

Ijapokuwa Umoja wa Mataifa na taasisi zake zimetoa maazimio zaidi ya 900 katika kipindi cha miaka 75 iliyopita kwa maslahi ya taifa la Palestina, lakini Israel imekataa kutekeleza lolote kati ya maazimio hayo. Marekani na washirika wake daima wamekuwa wakitumia kura ya kidhalimu ya veto dhidi ya jaribio lolote la kuitaka Israel kutekeleza maazimio hayo au kulaani mienendo miovu ya utawala huo. Kwa msingi huo, nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, zinashiriki katika uhalifu na jinai zisizo na kikomo za Israel na mateso yanayoendelea kuwapata watu wa Palestina.

Taarifa ya Hamas imeendelea kusema, viongozi wa Israel wametangaza upinzani wao dhidi ya kuundwa taifa huru la Palestina. Imesema: Mwezi mmoja kabla ya Kimbunga cha Al-Aqsa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alihutubia kikao cha Umoja wa Mataifa Septemba 2023, akionyesha ramani ya Palestina nzima, ikiwa ni pamoja na maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, kwa jina la Israel. Hata hivyo jamii ya kimataifa ilinyamaza kimya na haikuchukua hatua yoyote. 

Benjamin Netanyahu 

Mwishoni mwa taarifa yake, Hamas imetoa maswali kadhaa ikwa ni pamoja na kuuliza: 

Je, taifa la Palestina linapaswa kufanya nini mbele ya mipango ya kuyahudisha ardhi ya Palestina na kushadidi mashambulizi ya walowezi dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa?

Je, taifa la Palestina linapaswa kufanya nini ili kuulazimisha utawala ghasibu wa Israel kuwaachilia huru maelfu ya wafungwa wa Kipalestina kutoka katika jela zake?

Wapalestina wafanye nini ili kukomesha mzingiro wa kikatili wa Ukanda wa Gaza, ambao unaoua wananchi taratibu?

Je, taifa la Palestina linapaswa kufanya nini ili kukabiliana na ukatili na uhalifu unaofanywa na walowezi katika Ukingo wa Magharibi ambao umefikia kiwango kisicho na kifani?

Tags