Feb 22, 2024 04:46 UTC
  • Mashambulizi ya Israel dhidi ya Rafah

Hamjambo na karibuni katika Kipindi chetu wiki hii ambacho kitaangazia mashambulizi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya raia wa Palestina huko Rafah, kusini kwa Ukanda wa Gaza. Kuweni nami hadi tamati.****

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeanzisha mashambulizi katika mji wa Rafah, kusini mwa ukanda wa Gaza baada ya kushindwa kufikia malengo yake huko kaskazini na katikati mwa ukanda huo. 

Idadi kubwa ya wakazi wa Gaza wanaishi katika mji wa Rafah. Eneo la Rafah lina masafa ya takriban kilomita 65, na karibu Wapalestina milioni moja na nusu wanaishi katika mji huo. Hakuna shaka kuwa jamii ya sasa ya watu karibu milioni moja na nusu wakazi wa mji wa Rafah ni wakimbizi kutoka maeneo ya kaskazini na katikati mwa Gaza. Msongamano huu wa watu katika mji wa Rafah umelifanya eneo hilo litambuliwe kuwa eneo lenye msongamano mkubwa zaidi wa watu duniani. 

Wakimbizi wa Kipalestina katika mji wa Rafah 

Baada ya kusonga mbele huko kaskazini na katika baadhi ya maeneo ya katikati mwa Ukanda wa Gaza, jeshi la Israel lilitangaza kuwa sababu kuu ya kushambulia kivuko cha Rafah ni kukabiliana na Brigedi za Izzudin Qassam na kufanikisha operesheni ya kukomboa mateka wa Israel. Jeshi la Kizayuni limeanzisha mashambulizi makali katika kituo cha mwisho kilichowapa hifadhi wakimbizi wa Palestina na eneo salama pekee lililosalia kwa ajili ya utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Palestina kwa kisingizio cha kuwatafuta mateka wawili Israel katika eneo la Rafah. 

Hata hivyo mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Rafah yamekabiliwa na upinzani mkali wa jamii ya kimataifa. 

Jirani wa upande wa magharibi mwa Ukanda wa Gaza yaani Misri pia  imepinga uamuzi mpya wa baraza la mawaziri la mrengo wa kulia la Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu, wa kutuma mifumo yake ya ulinzi kaskazini mwa jangwa la Sinai na kuitishia Tel Aviv kuwa itasimamisha mkataba wa amani wa Camp David. 

Licha ya kupita siku 133 sasa tangu jeshi la Israel lianzishe mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza lakini baraza la mawaziri la dharura la utawala huo limeshindwa kufikia malengo yake kama kuiangamiza kikamilifu harakati ya Hamas, kukomboa mateka wa utawala wa Kizayuni na kubadili hali ya kijiografia ya Gaza.  

Mji wa Rafah una umuhimu mkubwa katika njia ya mawasiliano baina ya Gaza na ulimwengu wa nje kutokana na kuwa mwenyeji wa kivuko cha mpakani na kuwa kwake mhimili wa Philadelphia au mhimili wa Salahuddin, katika mpaka wa Ukanda wa Gaza na Misri. Katika miaka ya hivi karibuni, eneo hilo limekuwa mahali pa kukidhi mahitaji ya ndani ya Gaza.

Sasa, ikiwa imepita miezi minne tangu kuanza vita Ukanda Gaza, sehemu kubwa ya wakazi wa maeneo ya kaskazini na katikati mwa  ukanda huo wamelazimika kukimbilia katika mji wa Rafah ili kuhepa mashambulio ya kikatili ya Israel na kupata misaada ya kimataifa. Netanyahu na baraza lake la mawaziri ambalo limegonga mwamba na kushindwa kusambaratisha harakati za kupigania ukombozi za Wapalestina wamefungamanisha mafanikio au kushindwa kwao kuingamiza Hamas na mashambulizi ya kijeshi huko Rafah. Netanyahu anaelewa vyema kuwa, kupanua vita hadi katika mji wa Rafah kutazidisha mashinikizo ya kimataifa dhidi ya Israel ili istishe mashambulizi dhidi ya mji huo. Hasa ikizingatiwa kuwa, serikali ya Misri imeonya kuwa inaweza kusimamisha makubaliano ya Camp David iwapo vita vitafika huko Rafah. Katika mazingira kama hayo, Netanyahu anapata fursa ya kujitetea mbele ya wapinzani wake wa ndani kuwa, sababu ya kushindwa kwake katika vita vya Gaza na kuingamiza Hamas ni mashinikizo ya  kimataifa na kutokamilika mashambulizi dhidi ya Rafah.

Israel inadai kuwa moja ya njia kuu za kupeleka silaha na watu Ukanda wa Gaza ni mhimili wa Philadelphia. Viongozi wa Israel siku zote wanasema kupitia vyombo vya habari vya Kizayuni kwamba Rafah inapasa kukaliwa kwa mabavu ili kukamilisha mduara wa kuuzingira muqawama. 

Netanyahu ametangaza rasmi kuwa kushindwa jeshi la Israel kuingia Rafah kutakuwa na maana ya  kushindwa kikamilifu oparesheni ya kijeshi ya utawala huu. Wakati huo nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zimetoa taarifa zikitahadharisha kuhusu maafa ya binadamu huko Gaza. Msimamo kama huu kutoka kwa nchi hizo tatu kunaonyesha namna mashinikizo ya kimataifa yanavyozidi kuongezeka kwa ajili ya kusitishwa vita dhidi ya Gaza. 

Wakati huo huo kuna mtazamo kwamba, matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel yanalenga kuwaandaa kisaikolojia raia wa Israel ili wakubali kushindwa katika vita vya Gaza. 

Ni vyema kukumbusha hapa pia kwamba, mazungumzo ya kisiasa yameakhirishwa huko Qatar kutokana na kuanza oparesheni ya kijeshi ya Israel huko Rafah dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Palestina. Katika hali ambayo Marekani na Troika ya Ulaya pamoja na viongozi wa Doha na Cairo walikuwa kwenye mazungumzo ya kisiasa kwa lengo la kufanikisha usitishaji vita na kuachiwa huru mateka; jeshi la Israel lilifanya mashambulizi huko Rafah kwa kisingizio cha kuwakomboa mateka wake, suala ambalo limelalamikiwa vikali na wawakilishi wa Hamas. 

Kabla ya hapo wanamapambano wa Palestina walikuwa tayari wameafiki kwa masharti pendekezo la Paris na kutaka kufikiwa mapatano ya kudumu ya kusimamisha vita huko Gaza, kuachiwa huru mateka, kupatiwa dhamana yenye itibari na mwisho kuwekwa ramani ya njia kwa jaili ya ujenzi mpya wa eneo hilo.  

Hatua za Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni za kuvuruga juhudi zinazofanywa ili kufikiwa usitishaji vita huko Gaza zimemfamya hata Rais wa Marekani kuzitaja hujuma za karibuni za jeshi la Israel huko Gaza kuwa zimepindukia mpaka na kumtaja Netanyahu kuwa mpumbavu katika masuala ya kuendesha vita. 

Kwa kuzingatia kuwa Rafah ina mpaka na Misri na jangwa la Sinai, kuna mtazamo kwamba, lengo kuu la operesheni ya jeshi la Israel katika mji wa Rafah ni kukamilisha mpango wa kuwahamisha kwa lazima Wapalestina katika eneo hilo. Waziri wa Habari wa Israel ameeleza kuwa utawala huo unatekeleza sera inayojulikana kama "mkakati wa kijeshi wa kuangamiza kila kitu huko Ukanda wa Gaza au (scorched earth). Afisa huyo wa Israel anasema: Vita vikimalizika hakutakuwa na uwezekano wa kuishi tena mwanadamu katika eneo hilo. 

Naye Ripota wa haki za binadamu na vita dhidi ya  ugaidi wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na hatari ya kulazimishwa kuhama makazi yao. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa: Marekani haijatumia nyenzo zake zote  kuushinikiza utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza. 

Wakati huo huo Ayman Safadi Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan ametangaza kuwa jaribio lolote la kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni sawa na kutangaza vita dhidi ya nchi hiyo.

AymanSafadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan 

Hii ni katika hali ambayo, Marekani inajaribu kutumia sera hiyo ya Israel dhidi ya Gaza ili kuzishawishi nchi za Kiarabu kukubali takriban nusu ya wakazi wa eneo hilo kama wafanyakazi au raia licha ya Misri kupinga  mkakati huo wa kuwapatia makazi wakimbizi wa Gaza katika jangwa la Sinai.***** 

Tags