Mar 22, 2024 06:55 UTC
  • Lishe katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani (1)

Assalamu Alaykum Warahmatullhi Wabarakatuh. Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika kipindi chetu ncha leo cha Makala ya Wiki ambacho kinazungumzia lishe katika mwezi wa Ramadhani.

Ramadhani ni mwezi wa tisa wa mwaka wa Qamaria ambao funga imewajibishwa ndani yake kwa Waislamu. Katika Aya za Qur'ani Tukufu na Hadith za Mtume Muhammad (saw) na Maimamu watukufu baadaye yake, kumetajwa fadhila nyingi za mwezi huu ambao umetajwa kuwa ni mwezi wa ukarimu na ndani yake, Mwenyezi Mungu Karima amewaalika waja wake kwenye kitanga cha rehma na neema zake. Vilevile umetajwa kuwa ni msimu wa machipuo wa Qur'ani ambayo iliteremshwa katika mwezi huu. Vitabu kadhaa vya mbinguni kama vile Suhuf vya Ibrahim na Nuh (as), Taurati ya Musa (as) na Injili ya Isa (as) pia viliteremshiwa ndani ya mwezi wa Ramadhani.

Usiku adhimu wa Lailatul Qadr pia umo katika mwezi huu mtukufu. Ramadhani ndio mwezi pekee ambao jina lake limetajwa ndani ya Qur'ani na unatambuliwa kuwa ni mwezi wa ugeni na karamu ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake.

Inafaa kujua kwamba, pamoja na faida za afya ya kiroho za mwezi huu, kufunga swaumu pia kuna faida kubwa sana kwa afya ya mwili. Madaktari wanasema, kufunga wakati wa Ramadhani kunaruhusu mfumo wa mmeng'enyo kupumzika na kuzuia uchakavu wake. Kupumzika zaidi kwa mfumo wa mmeng'enyo kunaharakisha kazi ya kusambaza damu katika viungo vingine, hasa ubongo na mfumo wa neva. Vilevile husababisha kupungua kwa akiba ya awali ya mafuta katika mwili wa mtu aliyefunga, hata kwa watu wembamba au watu wenye uzito wa kawaida, na husababisha mafuta ya zamani ya mwili kuchomwa, na mafuta mapya na yanayofaa kuchukua nafasi yake. 

Katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, mlo mmoja huondolewa kwenye mlo wa kila siku wa watu waliofunga, na utaratibu wa chakula huwa wa milo miwili mikuu, ambayo ni futari na daku.

Kwa hivyo, kuwa na mpangilio wa chakula wenye mlingano katika mwezi wa Ramadhani huwafanya watu waliofunga waweze kunufaika kikamilifu na faida za kiroho ya mwezi huu na kuhitimisha kipindi hiki cha funga wakiwa na afya njema.

Lishe bora katika mlo wa Iftar

Lishe bora ni muhimu sana katika mwezi wa Ramadhani, haswa wakati wa mlo wa daku. Moja ya mambo yanayoshughulisha akili za watu wanaofunga ni kwamba, wakati wa daku tunapaswa kula nini ili tuweze kufunga kwa urahisi siku zote za mwezi bila ya mwili kupatwa na utapiamlo au udhaifu?

Kama tulivyosema, kufunga kuna faida nyingi kwa mwili wa mwanadamu, lakini siku ndefu bila kupata chakula au maji pia inaweza kusababisha matatizo kwenye mwili. Maumivu ya kichwa, kizunguzungu, udhaifu na uchovu ni baadhi ya matatizo ambayo unaweza kukutana nayo wakati wa Saumu ya Ramadhani. Jambo linaloweza kukusaidia kupunguza matatizo haya ni chakula sahihi cha wakati wa daku na lishe bora na yenye afya.

Wakati wa funga, mwili hutumia akiba ya kabohaidreti iliyohifadhiwa kwenye ini, misuli, na mafuta ili kudhamini nishati inayohitajika baada ya kalori zote za chakula kumalizika. Kwa hiyo, chakula cha daku kinapaswa kuwa cha afya na salama ili kushibisha mtu na kudhamini nishati muhimu ya mwili kwa saa kadhaa. Baadhi ya watu wanaamini kuwa, usipokula daku, hakuna shida itakayokupata, na kwamba wamefunga mara nyingi kwa njia hii bila shida yoyote. Huenda kidhahidi kusionekane tatizo lolote, lakini kwa mtazamo wa elimu ya lishe, sio tu kwamba ni muhimu kushibisha tumbo, bali pia kuna umuhimu sana wa kushibisha seli za mwili. Lengo la kushibisha seli sambamba na kushibisha tumbo kunakodhamini nishati ya mwili, ni kutayarisha mada zinazohitajiwa na mwili ikiwa ni pamoja na protini, vitamini, na madini. Mtu asiyekula daku mwezi Ramadhani huweka shinikizo kubwa juu ya mwili wake na hupata matatizo kwa ajili ya kudhamini nishati anayohitaji kwa siku. Inatupaswa kujua kwamba, matatizo haya hayana uhusiano wowote na kufunga Swaumu, bali ni matokeo ya lishe isiyofaa.       

Iftar au futari ndio mlo wa kwanza na muhimu zaidi baada ya kukamilisha Swaumu ya siku nzima, na vyakula vinavyotumiwa katika mlo huu vinapaswa kuwa na lishe inayofaa. Wakati wa futari inakupasa kuwa mwangalifu usiweke shinikizo kwenye mfumo wa mmeng'enyo na tumbo ambalo lilikuwa tupu kwa saa kadhaa. Ni bora kufuturu kwa kula kitu kama tende ili kuiga jinsi Mtume Muhammad (SAW) alivyokuwa akifungua.

Kuna udharura wa kufikiria chakula chenye kalori chache ambacho ni rahisi kusagika. Suala muhimu zaidi katika iftar ni kudhamini maji na sukari ya damu (Blood Glukose). Katika muktadha huo, tende ni mojawapo ya vyakula bora na muhimu zaidi vya kufuturu, ambavyo pia hudhamini glukozi na maji kwa mwilini wako. Pia, baada ya kufuturu, ni bora kunywa glasi ya maji kila baada ya saa moja hadi wakati wa kula daku.

Futari bora inapaswa kujumuisha vyakula vyenye potasiamu kama vile viazi mviringo au mbatata, tende, parachichi au ndizi. Pia, chakula cha futari mwezi Ramadhani kinapaswa kuwa na maji mengi na nyuzinyuzi ambazo hupatikana kwa kawaida katika matunda, mboga mboga, nafaka nzima, na kunde. Kwa mfano, matango, mboga ya saladi, na mboga nyingine na matunda ambayo yana nyuzi nyingi na maji mengi na ni chaguo nzuri kwa ajili ya chakula cha iftar.

Lishe bora ya iftar katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni muhimu 

Wapenzi wasikilizaji tunakutakieni Swaumu makbul, afya njema na kila la kheri hapa duniani na mwisho mwema huko Akhera....