Apr 05, 2024 05:58 UTC
  • Aya 30 Siku 30 (Uhuru na Mtu Huru katika Uislamu) 12

Asalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo na karibuni kuwa nami katika kipindi hiki maalumu cha Ramadhani ambacho kitatupia jicho uhuru na kuwa huru katika mtazamo wa Qur'ani Tukufu.

Siku tukufu za mwezi wa Ramadhani huleta habari njema kwenye nyoyo za waumini waliofunga. Katika mwezi huu, irada na nguvu ya kuchukua maamuzi ya Mwislamu huimarika zaidi na kumfanya aondokane na kuwa huru kutoka kwenye minyororo ya ndani ya nafsi na matamanio yake. Kuimarishwa huku kwa irada kunaweza kumfikisha mwanadamu kwenye uhuru kamili. Kuna watu wengi wanaodai kuwa huru na wanalingania uhuru kwa watu wengine, lakini wao wenyewe ni mateka na watumwa wa hawaa na matamanio ya nafsi zao. Ada ya kula na kunywa, tabia ya tamaa, kucheza kamari, kusengenya, kusema uongo, kunywa mvinyo n.k., vimewateka na kuwafunga minyororo na kuwatekka watu wa aina hii. Yumkini wakawa ni mabingwa na washindi katika nyanja za siasa na jamii, washindi vitani na hata katika mashindano ya michezo na kadhalika, lakini wakati huo huo wakawa mateka na wafungwa wa hawaa, matamanio ya nafsi, ufuska na kadhalika. 

Uhuru na mtu kuwa huru katika Uislamu 

Mtu anayejiondoa katika minyororo ya utawala wa silika za wanyama na kuacha kula na kunywa chakula chake halali, na akakanyaga matamanio haramu ya macho, masikio, ulimi, mkono, miguu na kadhalika kwa njia ya kufunga Swaumu, kwa hakika huwa anafanya jitihada za kujikomboa na kuwa mtu huru kwa maana yake halisi. Kwa msingi huo Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa uhuru na kuwa huru. Ni mwezi wa kuwa huru kutoka kwenye minyororo ya ada na tabia za kihayawani, kujikomboa kutoka kwenye matakwa ya tawala za kiimla, na kuwa huru kutoka kwenye makucha na udhibiti wa miungu bandia inayoamrisha maovu na kukataza mema. Aina hii ya uhuru ndio lengo takatifu la Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, na kama Quran Tukufu inavyosema, walitumwa kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu na kumuondoa kwenye minyororo ya nafsi, tawala za kimla na miungu bandia. Aya ya 157 ya Suratu Aaraf inasema: Ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika. Ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Taurati na Injili; Anawaamrisha mema na kuwakataza maovu, na anawahalalishia mazuri na kuwaharamishia vibaya, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.." 

Inatupasa kusema kuwa, matatizo mengi na makubwa ya mwanadamu yanasababishwa na kutofahamu uhuru halisi katika mtazamo wa Uislamu, au kutosimama imara na kuwa thabiti katika njia ya uhuru huo. Hivyo, wale ambao haufahamu maana ya uhuru huo au hawasimami imara na kuwa na istiqama katika njia ya uhuru huo, huangukia katika minyororo ya hawaa na matamanio ya nafsi au kwenye makucha ya watawala majabari na wanadamu wenye kiburi na majivuno na kuishia kujikomba kwao. Hii ni licha ya kwamba, Uislamu haumruhusu mwanadamu kunyenyekea na kurukuu mbele ya mwanadamu mwenzake au utawala wa kiimla na kidhalimu, badala ya Mwenyezi Mungu Mmoja 

Mfasiri mkubwa wa Qur'ani Tukufu, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai, anasema Mwenyezi Mungu SW ametahadharisha sana kuhusu madhambi mawili ndani ya Qur'an Tukufu. Madhambi hayo ni makubwa kuliko kunywa pombe, kucheza kamari, kuua nafsi bila ya haki na kadhalika, na Qur'ani Tukufu imetahadharisha kwa lugha kali sana kuhusu madhambi hayo kuliko dhambi ya kumuua mwanadamu. Madhambi hayo mawili ni "riba" na "kuwatawalisha maadui wa Mwenyezi Mungu katika jamii ya Kiislamu".

Allamah Muhammad Hussein Tabatabai

Katika Suratu Hud, baada ya kutaja historia ya kaumu za Nuhu, Hud, Salih, Ibrahim, Shuaib na Musa, Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 112 kwamba miungu yao haikuwafaa, basi wewe, ewe Mtume, simama ngangari uwe na istiqama. Basi, simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa, wewe na wale wanaoelekea kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote mnayotenda.

Nini maana ya istiqama katika maneno haya ya Mwenyezi Mungu? Aya inayofiatia inatoa jibu ikisema: Wala msiwategemee madhalimu, usije ukawapata moto. Na wakati huo hamtakuwa na walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, wala hamtasaidiwa.

Katika Aya hii inaeleweka kwamba, maana ya maneno ya Mwenyezi Mungu ya kuwa na istiqama na kutokiuka mipaka ni kutoegemea upande wa madhalimu na kutowategemea. Kwa sababu kuegemea na kuwategemea madhalimu, kunamfanya mwanadamu awe mshirika katika hatima yao mbaya.

Tunapodurusu na kutalii historia tunaona kuwa, waliookoka na kunusurika katika kaumu za Nabii Nuhu, Hud n.k., ni watu wachache tu ambao hawakuegemea au kuwategemea madhalimu. Maana ya kuegemea na kuwategemea madhalimu katika Aya hii si kuwa na imani nao pekee, bali kuwaamini kunakoambatana na kuwa nao na kuelekea upande wao. 

Katika Aya za kwanza na pili za Suratul Mumtahina, Mwenyezi Mungu anawaonya Waislamu wasikubali kuwa chini ya utawala wa maadui zake wanaojifanya miungu watu, ambao siku zote wanajaribu kuwaua, kuwatesa na kuwafanya watumwa wao na hatimaye makafiri. Inasikitisha kuona kwamba, wakati mwingine Waislamu- kwa kupenda au kutopenda- wanamwamini adui na kupoteza kila kitu, ikiwa ni pamoja na uhuru wao wa kidhahiri na kiroho. Tuna mifano kadhaa ya tawala za Waislamu ambazo ziliegemea, kuwaamini na kuwategemea maadui wa Allah SW na matokeo yake zilibezwa, zikafungwa minyororo kisiasa, kiuchumi, kijamii na kadhalima na kukosa uhuru na hatimaye zikaangamizwa na kuenguliwa, kama zilivyokuwa tawala za kina Muammar Gaddafi, Saddam Hussein, Zainul Abidin bin Ali, na Husni Mubarak.

Katika upande mwingine, kutokana na fikra yake ya kupigania uhuru, kujitawala na kusimama ngagari, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kupanua mipaka yake kutoka Kashmir hadi Bahari ya Mediterania, na haya ni mafanikio ambayo yamepatikana kwa njia ya "kutoa changamoto kwa adui". Mwanzoni mwa kuanzishwa utawala wa Kiislamu nchini Iran, tatizo la adui lilikuwa kwamba Iran isipate sen'genge kutoka popote pale katika vita ilivyolazimishwa miezi kadhaa tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu; Lakini leo tatizo la adui ni kwamba, makombora ya Iran yanaweza kupiga bara hadi bara jingine na kulenga shabaha kwa umakini mkubwa!

Mwaka wa 1979, changamoto ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa kubuni kwa urahisi iliyofeli ya "Operesheni ya Kucha ya Tai"  (Operation Eagle Claw) ili kuwakomboa mateka wa pango la ujasusi la Marekani nchini Iran; Lakini sasa, wakati askari wa vikosi bora vya jeshi la Marekani wanapokamatwa na wanajeshi wa Iran, hawana budi ila kulia kwa hofu. Wakati mmoja taifa la Iran lilihitaji makombora ya Libya na Syria, lakini leo makombora ya nchi hii yana neno na maamuzi muhimu katika vita vingi vya kikanda.

Iran ambayo haikuwa hata na uwezo wa kutengeneza seng'enge kabla ya ushindi wa Mapinduzui ya Kiislamu, sasa imepiga hatua kubwa na kuwa kati ya nchi zinazotajika duniani katika masuala kama teknolojia ya nyuklia, nano, anga za mbali, fizikia, teknolojia ya unajimu na utengeneza wa dawa nyingi muhimu za matibabu ya binadamu. Haya ni baadhi tu ya matokeo ya kusimama ngangari, imara, kuwa na istiqama na kutomwamini wala kumtegemea adui wa Allah SW kama inavyotufundisha Qur'ani Tukufu.

Qurani Tukufu