Ujumbe wa Hija wa Kiongozi Muadhamu 1445 Hijria
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, ametoa ujumbe kwa mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu wanaotekeleza ibada ya Hija ambapo ameutaja " Wito mzuri wa Ibrahim, ambao katika zama zote unawaita watu wote kwenye Al-Kaaba wakati wa msimu wa Hija, mwaka huu pia umevutia nyoyo za Waislamu kote duniani kwenye ngome ya Tauhidi na umoja.
Matini kamili ya ujumbe wa Hija wa Kiongozi Muadhamu ni kama ifuatavyo:
Bismillahir Rahmanir Rahiim
Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, na swala na salamu zimshukie mbora wa viumbe, bwana wetu Muhammad al-Mustafa na Aali zake watoharifu, maswahaba zake wateule, na wale wote waliowafuata kwa wema hadi Siku ya Kiama.
Kwa hakika wito wa kuvutia nyoyo wa Nabii Ibrahim ambao katika zama zote na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, umekuwa ukiwaita watu kuelekea al-Kabaa katika msimu wa Hija, mwaka huu pia umevutia nyoyo za makundi ya Waislamu kutoka pembe zote za dunia kujumuika katika kituo hiki cha Tauhidi na umoja. Umewezesha kujumuika pamoja umati huu mkubwa wa watu wenye rangi na lugha tofauti na hivyo kuwadhihirishia maadui na marafiki nguvu kubwa ya umma ya kiroho ya Uislamu.
Mtu anapozingatia mkusanyiko huu mkubwa wa watu na undani wa amali za Hija, bila shaka huwa ni chimbuko la nguvu na utulivu wa nyoyo kwa Waislamu na hofu na mfadhaiko kwa maadui na wenye chuki.
Hivyo halitakuwa jambo la kushangaza iwapo maadui na watu wenye nia mbaya dhidi ya Umma wa Kiislamu watalenga vipengele viwili hivi vya faradhi ya Hija kwa kujaribu kuharibu na kutilia shaka, ama kwa kuibua tofauti za kidini na kisiasa, au kudharau matakatifu na mambo ya kiroho ya faradhi hii.
Qur'an inaitambulisha Hija kuwa ni dhihirisho la uja, dhikri, unyenyekevu, dhihirisho la utukufu mmoja wa wanadamu, nembo ya kuboresha maisha ya kimaada na kimaanawi ya mwanadamuu, dhirisho la baraka na hidaya, nembo ya utulivu wa kiakhlaq (kimaadili), mapatano ya kivitendo baina ya ndugu na dhihirisho la chuki na kusimama kidete dhidi ya adui.
Kutadabari (kutafakari kwa kina) katika Aya zinazohusiana na Hija na kutaamali katika amali na matendo ya faradhi hii isiyo na mithili kunatuonyesha mambo na siri za ibada ya Hija kupitia muundo wake wa kina.
Nyinyi makaka na madada mnaotekeleza ibada ya Hija, hivi sasa mko katika uwanja wa kufanyia mazoezi ukweli na maarifa haya yenye nuru. Kurubisheni zaidi na zaidi fikra na amali zenu na mrejee nyumbani mkiwa mmepata tena utambulisho ambao umechanganyika na maarifa aali. Hii ndio ile adia na zawadi yenye thamani na ya kweli ya safari yenu ya Hija.
Mwaka huu kujibari na mushirikina kunapasa kuwa kukubwa kuliko huko nyuma. Maafa ya Gaza ambayo hayana mithili katika historia yetu ya leo, na kiburi cha utawala katili wa Israel, dhihirisho la unyama na ambao tabaani unaelekea kusambaratika, haujabakisha nafasi yoyote kwa mtu, chama, serikali na jamii ya Waislamu kuuzingatia au kuuvumilia. Kujibari na Mushirikina mwaka huu kunapasa kuwa ni zaidi ya msimu wa Hija na miqati na hivyo kuvuka mipaka ya wakati na zama kwa Waislamu kutoka miji na nchi mbalimbali kote duniani. Jambo hili linapaswa kuwa zaidi ya wanaofanya ibada ya Hija na kuwafikia watu wote.
Kujibari na kujiweka mbali na utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake hususan serikali ya Marekani kunapaswa kujionyesha kwa kauli na vitendo vya mataifa na tawala zao na hivyo kubana uwanja wa watesaji na wanyongaji.
Muqawama madhubuti wa Palestina na wananchi wenye subira na madhulumu wa Gaza ambao adhama yao, subira na kusimama kwao kidete kumeufanya ulimwengu kuwaenzi na kuwaheshimu, lazima uungwe mkono kwa kila njia.
Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu ushindi kamili na wa haraka, na ninawaombea nyinyi wapendwa Mahujaji, Hija maqbul. Na dua zenye kutakabaliwa za mtukufu Baqiyatullah-Imam Mahdi- (roho yangu iwe fidia kwake) ziwe kinga yenu.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh
Sayyid Ali Khamenei
4 Dhul-Hija 1445 H
22 Khordad 1403