Kwa dhambi gani ameuawa?
(last modified Wed, 20 Feb 2019 08:44:46 GMT )
Feb 20, 2019 08:44 UTC
  • Kwa dhambi gani ameuawa?

Mwaka 61 Hijria koo la mtoto mchanga aliyekuwa na umri wa miezi sita tuu wa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) likatwa kwa mshale wa adui wa Allah na Mtume wake aliyejulikana kwa jina la Harmala katika medani ya Karbala.

Dhulma iliyofanywa dhidi ya mtoto huyo mchanga imekuwa ushahidi wa uhalifu, unyama na ukatili mkubwa wa utawala wa Banii Umayyah hususan Yazid bin Muawiya. Ukatili huo umejikariri tena katika wiki chache zilizopita huko katika ardhi tukufu ya wahyi na ufunuo na karibu na mji mtakatifu wa babu yake Hussein, Madinatul Munawwarah kwa kuchinjwa mtoto Zakariya Bader al-Jabir aliyekuwa na umri wa miaka 6. Kuchinjwa kwa mtoto huyo kumedhihirisha tena ukatili wa itikadi na fikra za Kiwahabi na wale wanaojiita kuwa wanafuata masalafi. 

Ilikuwa habari ya kutisha na kushangaza sana kwa kila mwanadamu bila ya kijali dini, itikadi wala imani yake. Mama wa Zakariya Bader al-Jabir na mwanaye ambao ni wakazi wa eneo la  Al-Ahsa lenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia huko mashariki mwa Saudia Arabia walipanda gari la taxi wakielekea katika mji mtakatifu wa Madina kwa ajili ya kuzuru kaburi la Mtume wetu Muhammad (saw). Wakati wanapanda gari mama yake Zakaria alisema: Bismillahir Rahmanir Rahim.. akaomba dua kisha akawa anakariri kumswalia Mtume Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu. Dereva wa taxi alionekana kuguswa na maneno hayo ya mama yake Zakaria na baada ya mwendo kidogo alimuuliza: Wewe ni Shia? Mama wa Zakaria hakuficha itikadi yake na hapa ndipo dereva huyo alipoghadhibika na kusimamisha gari ghafla mkabala wa mkahawa mmoja ulioko karibu na eneo la al-Tilal. Dereva huyo aliingia mkahawani hapo akavunja kiyoo na kuchukua kipande chake, kisha akamchukua mtoto Zakaria kwa nguvu na kuanza kumchinja kwa kutumia kipande hicho cha kioo. Mama yake Zakaria alijaribu kukabiliana na mhalifu huyo bila ya mafanikio na aliishia kupiga mayowe na kuomba msaada lakini hakuna mtu aliyemwitikia. Mama alianguka chini na kuzimia kutokana na mauaji ya mwanaye tena mbele ya macho yake.

Zakariya Bader al-Jabir

Vyombo vya habari vimenukuu tukio hili la kutisha kwa riwaya mbalimbali lakini simulizi zote kuhusu uhalifu huu zinaonesha wazi kilele cha ukatili, uovu na fikra chafu za Kiwahabi zilizochochea mauaji ya mtoto huyo malaika kwa sababu tu ya itikadi za mama yake. Mtoto Zakaria ameuawa kwa kukatwa shingo kwa kipande cha kioo huko Saudi Arabia kwa sababu tu ni Mwislamu wa madhehebu ya Shia. 

Naam, Zakaria amechinjwa akiwa njiani kwenda kuzuru kaburi la Mtume wetu Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Madina na wale wanaojiita Waislamu.

Vyombo vya habari vya Saudi Arabia au vile vinavyolipwa na kufadhiliwa na utawala wa Riyadh vimefanya jitihada kubwa kujaribu kuficha uhalifu na ukatili huo unaotokana na itikadi na fikra za Kiwahabi. Kwa hakika kuuliwa kwa kwa mtoto huyo mchanga kwa kuchinjwa kwa kipande cha kioo kumeonesha tena uozo na upotovu wa itikadi za mashekhe wa kisalafi na Kiwahabi wa Saudi Arabia wanaochechea mauaji na ukatili dhidi ya Waislamu wasiofuata wala kuamini itikadi zao. Wasaudia wamekuwa wakifanya vitendo kama hivi kwa miaka mingi kupitia wawakilishi wa fikra zao kama Daesh, al Shabab, Boko Haram na al Qaida katika nchi kama Syria, Iraq, Yemen na Somalia ambako wanaua watu wasio na hatia kama watoto wadogo na kuwauza wanawake kama bidhaa masokoni. La kusikitisha zaidi ni kwamba, hayo yote yanafanyika kwa jina la Uislamu. 

Abdullah Issa alichinjwa na Daesh huko Halab (Aleppo) Syria

Kundi bandia la Kiwahabi kwa zaidi ya karne mbili sasa ambapo limekuwa likiharibu sura safi ya Uislamu na kuchafua thamani za dini hiyo tukufu. Mafundisho ya kundi hilo yanakinzana na mantiki na wala hayaoani na maumbile safi na asili ya mwanadamu. Uwahabi ni kundi ambalo tunaweza kusema kuwa, ni jipya na geni lililochipuka na kukulia huko Saudi Arabia. Kundi hilo lilienea kwa kasi katika miaka iliyopita kwenye maeneo mbalimbali ya dunia kutokana na misaada ya kifedha ya watawala wa kizazi cha Aal Saudi. Wafuasi wa kundi hilo wanajitambua kuwa ndio Waislamu pekee na Waislamu wa madhehebu nyingine ni makafiri na washirikina. Kwa sababu hiyo Mawahabi wanahalalisha kuwaua Waislamu wengine wasiofuata itikadi zao hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia. Ushahidi wa ukweli huu unashuhudiwa mara kwa mara ndani na nje ya Saudi Arabia ambako Mawahabi wamekuwa wakifanya ukatili wa kutisha kwa himaya na misaada ya wanasiasa na mashekhe wa Kisaudi. Mauaji ya mamia ya mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu katika tukio la Ijumaa Nyeusi tarehe 31 Julai 1987 ambao walipigwa risasi na polisi wa utawala wa Aal Saud katika mji mtakatifu wa Makka, vifo vya maelfu ya mahujaji kutoka nchi mbalimbali huko Mina katika ibada ya Hija tarehe 24 Septemba mwaka 2015 kutokana na uzembe wa maafisa wa Saudia, mauaji yanayofanywa dhidi ya watoto na wanawake wa Syria, Iraq na Yemen kwa misaada ya kifedha na kisiasa ya Saudia kwa makundi ya kigaidi na Kiwahabi kama Daesh yote haya ni mifano midogo ya uovu wa fikra na itikadi za Kiwahabi zinazosambazwa na kuenezwa na mashekhe wa Saudia.

Maelfu ya mahujaji waliaga dunia Mina 2015.

Walimwengu bado wanakumbuka ukatili uliofanywa na utawala wa Saudi Arabia dhidi ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala huo, Jamal Khashoggi aliyekamatwa ndani ya ubalozi wa utawala huo katika mji wa Istanbul huko Uturuki kisha akauawa kikatili na maafisa wa serikali ya Riyadh wakisimamiwa na balozi wa nchi hiyo. Mwili wa mwandishi huyo ulikatwa vipande vipande na kupelekwa kusikojulikana. Kuchinjwa shingo ya mtoto Zakariya Bader al-Jabir mbele ya macho ya mama yake mzazi kunazidisha uzito wa faili chafu na jeusi la watawala wa Saudia na fikra potofu za mashekhe wa Kiwahabi wa nchi hiyo. Hususan pale inapoeleweka kuwa, maafisa wa serikali ya Saudi Arabia hawakutoa hata taarifa ya kulaani walau kwa maneno tu ukatili huo ambao umegubika vyombo vya habari na kuwashtua watu wengi kote duniani.

Mauaji haya ya kutisha yamefanyika katika nchi inayojinadi kuwa ni kitovu cha Uislamu ambao unathamini sana uhai wa mwanadamu na kutambua kitendo cha kutoa roho ya kiumbe huyo kuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa. Aya ya 32 ya Suratul Maida inasema: "Anaye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uovu katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu (mmoja) na mauti ni kama amewaokoa watu wote…"  

Vilevile aya ya 93 ya Suratu Nisaa inasema: Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa.

Hapa linakuja swali kwamba, ni vipi mwanadamu anatoa roho ya mwanadamu mwenzake tena bila ya kosa lolote?

Katika upande mwingine maumbile safi na asili yaliyowekwa ndani ya nafsi ya mwanadamu yanasifu na kupongeza maadili mema na mienendo mizuri na kulaumu na kulaani tabia na mienendo mibaya. Kutunza amana, kusema ukweli, kuwa uaminifu na uungwana ni sifa zinazopendwa na kusifiwa katika jamii, dini, madhehebu na mielekeo yote ya wanadamu ambazo pia zinachukia, kulaani na kukemea urongo, ukatili, hadaa na kufanya hiyana katika amana. Hapa linakuja swali jingine kwamba, ni kina nani wanaochafua fikra na maumbile safi na asili ya watu na kuwachochewa kufanya ukatili unaotikisa dhamira za wanadamu kama mauaji ya mtoto mdogo mwenye umri wa miaka sita Zakaria al Jabir tena kwa kukata shingo yake kwa kipande cha kioo? Na ni itikadi za aina gani hizo zinazowafundisha watu kuwaua kikatili wanadamu wenzao kwa sababu tu wanatofautiana nao kifikra na hawafuati fikra na itikadi zao za kitakfiri? Je, mashekhe wa Kiwahabi wa Saudi Arabia wanaohalalisha damu za Waislamu wa madhehebu ya Shia na kutangaza kwamba mtu anayewaua Waislamu hao anapata thawabu na kuingia peponi hawajasoma aya za Qur'ani tukufu zinazosisitiza kwamba mtu anayeua mwanadamu mwenzake bila ya dhambi au kosa lolote ni kana kwamba ameua wanadamu wote?

Itikadi za Kiwahabi zinachochea mauaji na ukatili dhidi ya Waislamu duniani

Ni itikadi za aina gani hizo zinazowafundisha wafuasi wake kumuua Muislamu anayekwenda Madina kuzuru kaburi la Mtume Muhammad (saw) na kudhihirisha mapenzi yake kwa mtukufu huyo na Aali na kizazi chake kwa sababu tu hakubaliani na fikra za Kiwahabi. Inna lillah Wainna ilayhi Rajiuuun.

Inasikitisha sana kuona kwamba, jumuiya za kimataifa eti za kutetea haki za binadamu zimenyamazia kimya ukatili huo wa kutisha. Shirika la kutetea haki za binadamu la Shia Rights Watch ambalo ndilo pekee lililolaani ukatili huo limeandika kuwa: Waislamu wa madhehebu ya Shia wanakandamizwa na kuuawa kwa kiwango cha kutisha nchini Saudi Arabia na kwamba wanaharakati wengi wa Kishia wanashikiliwa katika korokoro za utawala huo. Gazeti la The Sun la Uingereza pia limeripoti kuwa, maafisa wa serikali ya Saudi Arabia wamejaribu kuficha uhalifu huo kwa kudai kuwa dereva aliyefanya mauaji hayo ya kutisha anasumbuliwa na matatizo ya kinafsi. Madai haya ya maafisa wa serikali ya Saudia yanawakumbusha walimwengu madai yanayotaka kushabihiana na hayo yaliyotolewa na serikali ya Riyadh baada ya mauaji ya Jamal Khashogghi ndani ya ubalozi wa Saudia nchini Uturuki kwa kudai kuwa, maafisa 15 wa serikali waliofanya uhalifu huo wakisimamiwa na balozi wa nchi hiyo, walifanya mauaji hayo bila ya idhini ya serikali!

Uchunguzi: Bin Salman aliamuru mauaji ya Khashoggi

Shahidi Zakaria alikuwa mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 6 ambaye hakujua lolote kuhusiana na hitilafu za kiitikadi na kimadhehebu. Zakaria ameuawa kwa kukatwa shingo katika nchi yake mwenyewe na akiwa njiani kwenda kuzuru kaburi la Mtume Muhammad (saw), babu wa Hussein bin Ali ambaye pia aliuawa na wahalifu wa kizazi cha Banii Umayyah mwaka 61 Hijria kwa njia hiyo hiyo ya kukatwa shingo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu SW amfufue Zakaria pamoja na Mtume na Aali zake watoharifu na awape subira na uvumilivu wazazi wake. Vilevile tunamuombea shifaa na ahueni mama yake Zakaria ambaye vyombo vya habari vinasema alikuwa mahututi katika hali ya kupeza fahamu kutokana na mshtuko mkubwa uliompata baada ya kushudia kwa macho mauaji ya kipenzi chake.