Sudan yaendelea kushuhudia mapigano makali katika miji mbalimbali
Mapigano makali yameendelea kuripotiwa katika miji mbalimbali ya Sudan baina ya jeshi la nchi hiyo na kikosi cha usaidizi wa haraka huku kukiwa hakuna ishara za kumalizika vita hivyo hivi karibuni.
Mapigano hayo yanashadidi sambamba na kufeli juhudi za kieneo na kimataifa za kuleta upatanishi na kuhitimisha vita hivyo ambavyo vimesababisha uharibifu na mauaji huku idadi ya wakimbizi ikiongezeka kila siku.
Vita na mapigano ya kuwania madaraka nchini Sudan yalianza Aprili 15 kati ya jeshi linaloongozwa Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vinavyoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo; na hatua za upatanishi wa kimataifa zilizofanywa kwa lengo la kuhitimisha mapigano hayo kwa kuzileta pande hasimu kwenye meza ya mazungumzo hadi sasa bado hazijazaa matunda.
Watu wasiopungua 3,000 wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kukimbia makazi yao tangu ghasia hizo zilipoanza mapema mwaka huu.
Jenerali Mohammad Hamdan Dagalo, kamanda wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vinavyopigana vita na jeshi la taifa nchini Sudan ametangaza kuwa, vikosi vyake havitaruhusu mabaki ya utawala wa zamani kuchukua madaraka tena nchini humo.
Umoja wa Mataifa unasema, idadi ya wakimbizi wanaowasili Sudan Kusini kutokea Sudan inatabiriwa kuendelea kuongezeka kutokana na kuwa, mgogoro wa vita vya ndani huko Sudan ambayo ni nchi ya tatu kwa ukubwa wa ardhi barani Afrika bado haujapatiwa ufumbuzi.