Sudan: Madai ya Wamagharibi dhidi yetu hayana msingi
Sudan imezishutumu nchi za Magharibi kwa kuingiza siasa katika suala la misaada ya kibinadamu na kulilaumu jeshi la Sudan na serikali ya nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika kwa 'kuzuia misaada.'
Serikali ya Sudan imesema hayo kufuatia tamko la pamoja la Oktoba 18 la Uingereza, shirika la USAID la Marekani, Norway, Sweden, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Ireland, Uswisi, Canada, na Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayesimamia migogoro, ambalo lilitoa wito wa kuondolewa vizingiti vinavyozuia ufikishaji wa misaada nchini Sudan.
Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imeishutumu taarifa hiyo ya pamoja ya Wamagharibi na kuitaja kuwa ya upendeleo, ikidai kuwa hakuna ushahidi wa serikali ya Khartoum kuzuia kwa makusudi shughuli za kibinadamu. Wizara hiyo imekanusha kuwa mamlaka za serikali zilizuia kwa makusudi utoaji wa viza za kuingia na vibali vya usafiri kwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.
Hivi karibuni pia, serikali ya Sudan ilikosoa vikali taarifa ya majuzi ya Marekani iliyoituhumu serikali ya Khartoum kwamba inazuia watu nchi humo kufikishiwa misaada ya kibinadamu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilisema, tuhuma za Marekani dhidi ya Jeshi la Taifa la Sudan SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF ni za urongo na hazina msingi wowote.
Haya yanajiri huku vita vya kuwania madaraka vikiendelea kuchachamaa nchini Sudan. Juhudi za kieneo na kimataifa za kuzishawishi pande mbili hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo na kutatua tofauti zao hazijafua dafu mpaka sasa.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), watu zaidi ya 24,000 wameuawa tangu mapigano baina ya pande hizo mbali yaanze nchini Sudan katikati ya Aprili mwaka uliopita 2023.