Mahakama ya ICC yatoa waranti wa kukamatwa Netanyahu na Gallant
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na aliyekuwa waziri wake wa vita Yoav Gallant, wakituhumiwa kutenda jinai za vita.
Kwa mujibu wa waranti huo wa ICC, Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant ambao wanatajwa na duru nyingi kuwa wahusika wakuu wa mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza, wanatuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na vita vyao vya miezi 13 huko Gaza.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imesema katika waranti huo kwamba, Netanyahu na Gallant wanakabiliwa na makosa ya uhalifu wa kivita ambao wameyafanya kati ya tarehe 8 Oktoba mwaka 2023 hadi tarehe 20 ya mwezi Mei mwaka huu.
Waranti huo unataka pia kukamatwa baadhi ya maafisa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamuu ya Palestina HAMAS.
Mwezi Mei mwaka huu, Karim Khan, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), alitaka itolewe hati ya kumkamata waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, na waziri wake wa vita Yoav Gallant kwa sababu ya kutenda jinai katika vita vya utawala huo dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza huko Palestina.
Hati ya kukamamatwa Netanyahu na Gallant imetolewa na mahakama ya ICC katika hali ambayo, mahakama hiyo imekuwa ikiandamwa na mashinikizo ili kuizuia isitoe hati ya kukamatwa watenda jinai hao wa Israel.