Waafrika Kusini wamjia juu Trump kwa kuongopa kwenye kikao na Ramaphosa
Wananchi wa Afrika Kusini wameeleza kughadhabishwa na madai ya uwongo yaliyobuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa mazungumzo yake na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini katika Ikulu ya White House.
Katika kikao hicho cha Jumatano, Trump hakuheshimu protokali za kidiplomasia na aliikosoa vikali serikali ya Afrika Kusini kwa kile alichodai kuwa ni mashambulizi dhidi ya watu weupe nchini Afrika Kusini.
Waafrika Kusini mitandaoni na mitaani wamekosoa vikali madai hayo ya uwongo ya Trump, ya kuwepo mauaji ya halaiki ya wazungu nchini kwao, na wengi wao walishangaa iwapo safari ya Ramaphosa ya Washington ilikuwa na manufaa yoyote.
"Sidhani kama ulikuwa wito sahihi. Sidhani kama tunahitaji kujieleza kwa Marekani," Sobelo Motha mwenye umri wa miaka 40, mwanachama wa muungano wa wafanyakazi, amesema katika mitaa ya Johannesburg.
Kijana mwingine ambaye hakutaja jina lake amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, "Sisi ... tunajua hakuna mauaji ya kimbari ya wazungu. Kwa hiyo kwangu mimi, safari hiyo haikuwa na maana yoyote."
"Nadhani kampeni ya upotoshaji ya makundi mbalimbali ya mrengo wa kulia na makundi mbalimbali ya Waafrikana imefanikiwa sana," mwandishi mzungu wa Afrika Kusini, Pieter du Toit aliiambia Reuters.
Wakati wa mkutano huo katika Ikulu ya White House, Trump alimwonyesha Ramaphosa picha alizodai ni ushahidi wa ukatili dhidi ya wakulima wa kizungu huko Afrika Kusini.
Hata hivyo, shirika la habari la Reuters limekanusha vikali madai hayo ya Trump, likisema kuwa picha iliyotumiwa na Trump ni ya shirika hilo, imetumika ndivyo sivyo kupotosha umma.
Reuters imesema: Picha hiyo ilitokana na video iliyowaonyesha wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wakibeba mifuko ya miili katika mji wa Goma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Trump amedanganya kwa kutumia picha hiyo kama ushahidi wa 'mauaji makubwa' ya Wazungu Afrika Kusini.