Bunge la Seneti DRC lamuondolea Joseph Kabila kinga ya kutoshtakiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126738-bunge_la_seneti_drc_lamuondolea_joseph_kabila_kinga_ya_kutoshtakiwa
Bunge la Seneti la katika Jamhuri ya Kidemokkrasia ya Congo limeondoa kinga ya kutoshtakiwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila, na kuufuungua njia ya kufunguliwa mashtaka dhidi yake.
(last modified 2025-05-23T08:53:24+00:00 )
May 23, 2025 08:53 UTC
  • Bunge la Seneti DRC lamuondolea Joseph Kabila kinga ya kutoshtakiwa

Bunge la Seneti la katika Jamhuri ya Kidemokkrasia ya Congo limeondoa kinga ya kutoshtakiwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila, na kuufuungua njia ya kufunguliwa mashtaka dhidi yake.

Kabila ambaye pia ni seneta wa maisha, anatuhumiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita, na kuunga mkono kundi la waasi la M23 ambalo liliteka miji mikubwa Mashariki mwa Congo mapema mwaka huu.

Kwa jumla, Maseneta 88 walipiga kura ya kuunga mkono kushitakiwa kwake, ni watano pekee waliopinga kuondolewa kinga hiyo huku kura nyingine tatu zikibatilishwa. Joseph Kabila ambaye aliondoka nchini 2023 hakufika mbele ya seneti kujitetea kabla ya kura ya leo.

Anakuwa Mkuu wa kwanza wa zamani wa nchi kushtakiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita na mashtaka yanayohusiana nayo.

Uamuzi huo sasa unatoa nafasi kwa mahakama ya kijeshi kuanzisha kesi dhidi yake.

Mwezi uliopita, Waziri wa Sheria alipeleka suala hilo kwenye mahakama za kijeshi ili kuanzisha kesi dhidi ya mkuu huyo wa zamani wa nchi "kwa ushiriki wake wa moja kwa moja" katika vuguvugu la M23 katika muktadha wa kushadidi mzozo mashariki mwa DRC.

Mwanasheria mkuu wa jeshi la Kongo kisha aliwasilisha ombi kwa Baraza la Seneti ili kuondoa kinga yake, akimtuhumu kwa "uhaini, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na kushiriki katika harakati za uasi."

Kulingana na wafuatiliaji wa mambo, kesi yoyote itakayofunguliwa dhidi yake huenda ikazidisha machafuko kwenye taifa hilo ambalo tayari linakabiliwa na mizozo ya kisiasa, kutokana na mashambulizi yanayofanywa na waasi wa M23 huko mashariki mwa Kongo, wanasema wachambuzi.

Kabila aliyehudumu kwa miaka 18 kama rais alikuwa na kinga ya kutoshitakiwa. Na bado ana ushawishi mkubwa kwenye uwanja wa siasa wa Kongo, hata baada ya serikali ya muungano na Tshisekedi kuvunjika miaka miwili iliyopita.