Sardasht; Jeraha Lisilosahaulika Duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139504-sardasht_jeraha_lisilosahaulika_duniani
Julai 28, 1987, imewekwa alama katika kalenda rasmi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama kumbukumbu ya moja ya jinai za kivita za kutisha dhidi ya ubinadamu. Siku hii, inakumbushia shambulio la kikatili la mabomu ya kemikali katika mji wa Sardasht lililofanywa na utawala wa Baath wa Iraq; jinai ambayo ilitekelezwa kwa uungaji mkono na kimya cha aibu cha madola ya Magharibi.
(last modified 2026-06-29T07:55:18+00:00 )
Jun 29, 2026 07:49 UTC
  • Sardasht; Jeraha Lisilosahaulika Duniani

Julai 28, 1987, imewekwa alama katika kalenda rasmi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama kumbukumbu ya moja ya jinai za kivita za kutisha dhidi ya ubinadamu. Siku hii, inakumbushia shambulio la kikatili la mabomu ya kemikali katika mji wa Sardasht lililofanywa na utawala wa Baath wa Iraq; jinai ambayo ilitekelezwa kwa uungaji mkono na kimya cha aibu cha madola ya Magharibi.

Katika siku hiyo iliyokuwa na joto kali lililoandamana na kimya, ndege ya kijeshi ya utawala wa Saddam ilidondosha mabomu ya gesi ya haradali katika maeneo manne ya makazi yenye msongamano mkubwa wa watu katika mpaka wa Iran na Iraq, na kugeuza maisha ya kawaida ya zaidi ya raia elfu kumi na mbili kuwa ndoto ya jinamizi isiyo na mwisho.

Ghafla, vichochoro na mitaa ilijaa miili ya watu na majeruhi walioanguka chini huku wakipatwa na malengelenge, wakikohoa damu na kupumua kwa matatizo, bila kufahamu chanzo cha shambulio hilo. Maafa haya yaliweka jina la Sardasht katika historia ya mwanadamu kama mji wa kwanza duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia, kushambuliwa moja kwa moja na kwa kiwango kikubwa, kwa silaha za kemikali.

Karibu miongo minne baada ya tukio hilo chungu, manusura wengi wa tukio hilo bado wanateseka kutokana na madhara yake ya kimwili na kisaikolojia. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa katika siku ya shambulio hilo la kinyama na siku zilizofuata, zaidi ya wakazi mia moja wa Sardasht walipoteza maisha, na idadi ya waathirika wa kemikali ikafikia takriban elfu nane. Hata hivyo, idadi hii ni sehemu tu ya unyama huo. Gesi ya haradali, pamoja na athari zake za kudumu na zinazoendelea, imekuwa ikiharibu taratibu mapafu, macho na mifumo ya kinga ya waathirika kwa miaka mingi. Maelfu ya wahanga wa shambulio la kemikali la Sardasht bado wanakabiliwa na matatizo ya kupumua, vidonda vya macho, utasa, maradhi ya ngozi na msongo mkubwa wa mawazo.

Ukubwa wa maafa ya shambulio la kemikali la Sardasht huenda likazidi maafa ya kawaida katika uwanja wa vita na idadi ya wahanga. Moja ya nukta muhimu katika jinai hiyo ya kinyama ni ushiriki wa serikali za Magharibi katika kuandaa, kuunga mkono na kukaa kimya mbele ya jinai hiyo ya Saddam. Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 39 ya maafa hayo, amesema: "Sardasht si mji tu; ni nembo ya ukandamizaji uliofanywa dhidi ya taifa ambalo lilikuwa mhanga wa silaha zilizopigwa marufuku lakini pamoja na hayo halikulegeza msimamo hata kidogo katika kukabiliana na ukandamizaji." Amekumbusha kwamba historia inathibitisha wazi kwamba uungaji mkono na kimya cha baadhi ya serikali za Magharibi hususan Marekani, Ujerumani na Uingereza katika kuupa utawala wa Saddam silaha za maangamizi ya umati na matumizi makubwa ya silaha hizo dhidi ya wananchi wa Iran na hata dhidi ya mji wa Halabja, wa Iraq yenyewe, ni jambo linalothibitisha wazi ushiriki wa nchi hizo katika maafa hayo ya kutisha. Nyaraka na ripoti za kuaminika kutoka mashirika ya kimataifa zinaonyesha kwamba makampuni ya Magharibi ya kemikali na kijeshi yalimpa dikteta huyo mtenda-jinai wa Iraq malighafi, vifaa vya hali ya juu na teknolojia ya kuzalisha gesi za sumu, na wakati huo huo, kuzuia kupitishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, azimio lolote ambalo lingepiga marufuku utekelezaji wa jinai hiyo. Undumakuwili na ushiriki huu katika jinai sio tu kwamba ulikejeli sheria za kimataifa, bali pia uliandaa mazingira ya kukaririwa jinai kama hiyo katika siku zijazo. Katika ujumbe wake kwa mnasaba huo, Araqchi ameashiria hujuma za hivi karibuni za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na kusema, "ni kana kwamba gurudumu la wakati linakariri mtihani huo huo mkubwa baada ya miongo kadhaa. Mtihani kati ya ukweli na uwongo, nuru na giza, na kati ya utu wa mwanadamu na uovu."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran huku akikumbusha kwamba kimya cha serikali nyingi duniani hii leo mbele ya ukiukaji wa wazi wa misingi ya ubinadamu ni mwendelezo ule ule wa jinai ya Sardasht, amesisitiza azma ya Iran ya kufuatilia haki zake kuhusu suala hili katika taasisi na majukwaa ya kimataifa. Ikiashiria Mkataba wa Geneva wa mwaka 1925 wa Kuzuia Silaha za Kemikali, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran inasisitiza kuwa wahusika wote wa jinai hiyo wanapaswa kuwajibishwa kisheria katika vyombo vya kimataifa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali katika zama hizi, imekuwa na nafasi muhimu katika kuandaa Mkataba wa Kuzuia Silaha za Kemikali na daima imekuwa katika mstari wa mbele wa juhudi za kubuni ulimwengu usio na silaha za maangamizi ya umati.

Leo, Sardasht ni ushuhuda ulio hai wa mapambano kati ya haki na batili na mtihani mkubwa kwa dhamiri ya jamii ya kimatifa. Miaka thelathini na tisa imepita tangu siku hiyo, lakini maelfu ya wahanga bado wanasubiri kutendewa haki na kupata uponyaji, ambapo inasikitisha kuona kwamba jamii ya kimataifa inaendelea kukaa kimya mbele ya jinai hiyo ya kihistoria, na kuandaa mazingira ya kukaririwa jinai nyingine kama hiyo. Mfano wa wazi ni mauaji ya umati na jinai zinazoendelea kufanywa kila siku na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Ujumbe wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa mnasaba wa kukumbuka shambulio la bomu la kemikali huko Sardasht ni wa kukomeshwa kimya hiki na kuzingatiwa utu wa mwanadamu mkabala wa uonevu na ubeberu, ambapo hakutakuwa tena na taifa au mwanadamu atakayewahi kuwa mhanga wa vita, ugaidi, na silaha za maangamizi ya umati, na ulimwengu kusimama kwenye msingi wa haki, ukweli, na kuheshimiana.