Ramaphosa amfumba mdomo Donald Trump
Rais wa Afrika Kusini, ambaye alikuwa mgeni wa rais wa Marekani katika Ikulu ya White House amejibu shutuma kali za Trump dhidi ya serikali ya Afrika Kusini kwa kumpa majibu mazito yaliyomfumba mdomo rais huyo mwenye kiburi wa Marekani.
Donald Trump alikuwa mwenyeji wa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini katika Ikulu ya Marekani jana Jumatano.
Wakati wa mazungumzo yao na mbele ya kamera za vyombo vya habari, Trump hakuheshimu protokali za kidiplomasia kama kawaida yake na aliikosoa vikali serikali ya Afrika Kusini kwa kile alichodai kuwa ni mashambulizi dhidi ya watu weupe nchini Afrika Kusini. Wakati wa mkutano huo, Trump alimwonyesha Ramaphosa picha alizodai ni ushahidi wa ukatili dhidi ya wakulima wa kizungu huko Afrika Kusini.
"Haya ni mawe ya makaburi - zaidi ya elfu moja - ya wakulima wazungu," Trump alisema. "Misalaba inaweza kuonekana pande zote mbili za barabara." Lakini Ramaphosa amemjibu kwa kumwambia, kwanza mimi sina ndege ya kukupa zawadi na pia amemuuliza Trump, video hiyo imechukuliwa wapi? "Sijawahi kuiona," amesema.
Rais wa Afrika Kusini ameendelea kusema, "Samahani, sina ndege ya kukupa zawadi." Trump akajibu kwa kusema, na ungelinipa ningeliipokea.
Ikumbukwe kuwa, siku chache zilizopita, katika ziara ya rais wa Marekani katika nchi za Kiarabu za eneo hili la Asia Magharibi, Qatar ilimzawadia Trump ndege aina ya Boeing 747, inayojulikana kwa jina la Flying Palace. Ndege hiyo ina thamani ya dola milioni 400 za Kimarekani.