Wafanyakazi wawili wa ubalozi wa Israel wauawa kwa kupigwa risasi Washington
Wafanyakazi wawili wa ubalozi wa utawala haramu wa Israel mjini Washington wameuawa kwa kupigwa risasi jana jioni, nje ya Jumba la Makumbusho la Kiyahudi katika mji mkuu wa Marekani. Hayo ni kwa mujibu wa maafisa na vyombo vya habari.
Tayari Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel Benjamin Netanyahu ameagiza kuimarishwa kwa usalama balozi zote za Israel kote ulimwenguni.
"Wafanyakazi wawili wa ubalozi wa Israeli wameuawa kiholela jioni hii karibu na Jumba la Makumbusho la Kiyahudi huko Washington. "Tunachunguza kikamilifu kisa hiki" Waziri wa Usalama wa Ndani Kristi Noem ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Kulingana na ripoti za awali kutoka kwa meya na Polisi wa mji wa Washington, karibu saa 3:00 usiku saa za Washingtoni, wakati Jumba la Makumbusho la Kiyahudi la mji mkuu, lililoko karibu na Capitol, lilikuwa likiandaa hafla ya wanadiplomasia vijana wa Israel, mtu wa miaka thelathini, aliyetambuliwa kama Elias Rodriguez, kutoka Chicago, huko Illinois, amewafyatulia risasi wanandoa nje ya jumba la makumbusho, na kupiga kelele "Free Palestine" ikimaanisha kwa Kiswahili "Palestina huru". Alikamatwa na silaha yake na vyombo vya uslama. Kwa hivyo hakuna hatari tena katika eneo la tukio, anaripoti mwandishi wetu huko Washington, Guillaume Naudin.
Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump pia amejibu haraka. "Mauaji haya ya kutisha huko Washington, ambayo ni wazi yanachochewa na chuki dhidi ya Wayahudi, lazima yakome, SASA!" " amesema kwenye mtandao wake wa Truth Social. "Chuki na itikadi kali hazina nafasi nchini Marekani," ameongeza. "Ilikuwa ni kitendo cha ukatili, chuki dhidi ya Wayahudi. "Msijidanganyi: tutawapata waliohusika na kitendo hiki kiovu na kuwafikisha mahakamani," ameandika Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kwenye mtandao wa kijamii wa X.