Bunge lapasisha makubaliano ya kimkakati ya Iran na Russia
(last modified Wed, 21 May 2025 10:10:35 GMT )
May 21, 2025 10:10 UTC
  • Bunge lapasisha makubaliano ya kimkakati ya Iran na Russia

Wajumbe wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) wamepasisha rasimu ya Mkataba wa Ushirikiano Kamili wa Kimkakati kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Shirikisho la Russia.

Katika kikao cha wazi kilichofanyika leo Jumatano, Bunge la Iran limefanya mapitio ya rasimu ya Mkataba wa Ushirikiano Kamili wa Kimkakati kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Shirikisho la Russia na wabunge wamekubaliana na maelezo yaliyomo kwenye muswada huo kwa kura 192 za ndio, kura 5 za kupinga, na 2 kujizuia kupita kura kati ya jumla ya wabunge 211 waliohudhuria kikao hicho.

Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: Mkataba wa Ushirikiano wa Kimkakati na wa Kina kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Shirikisho la Russia, unaojumuisha utangulizi na vifungu (47) kama vilivyoambatanishwa, umepashiwa pamoja na hati zake.

Bunge la Iran

 

Sehemu nyingine ya taarifa ya Bunge la Iran imesema: Kanuni za sabini na saba (77), mia moja na ishirini na tano (125) na mia moja na thelathini na tisa (139) za Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimepasisha Mkataba wa Ushirikiano wa Kina wa Kimkakati kati ya Iran na Russia.

Mbunge Alireza Salimi alipendekeza kuondolewa kifungu cha maneno kinachosema “au kurekebisha” katika maandishi ya muswada huo kutokana na kukinzana na ibara ya 85 ya Katiba inayolinyima Bunge mamlaka hayo, lakini hilo halikukubaliwa na wabunge. 

Azimio hilo la Bunge la Iran sasa litapelekwa mbele ya Baraza la Kulinda Katiba la Jamhuri ya Kiislamu ili kuidhinishwa.