Yemen yaiwekea mzingiro Bandari ya Haifa ili kuiunga mkono Palestina
(last modified Wed, 21 May 2025 02:26:03 GMT )
May 21, 2025 02:26 UTC
  • Yemen yaiwekea mzingiro Bandari ya Haifa ili kuiunga mkono Palestina

Yemen imetangaza habari ya kuifunga Bandari ya Haifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kupachikwa jina bandia la Israel, ili kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kujibu mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa rasmi iliyorushwa hewani na Al Mayadeen jana Jumanne, Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen, amenukuliwa akizionya kampuni zote za usafiri wa baharini ambazo meli zao zimetia nanga au zinaelekea Haifa, na kuzitaka zichukulie tangazo na maonyo hayo kwa uzito.

Kadhalika kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Al-Masirah, Jeshi la Yemen limezionya vikali kampuni za meli zinazoelekea Haifa, na kuzitaka kuzingatia tangazo hilo.

Hatua hiyo imekuja kutokana na ongezeko la mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Gaza na kampeni ya njaa ya utawala hup pandikizi dhidi ya Wapalestina, imeongeza taarifa hiyo.

Jenerali Saree amesisitiza kuwa, operesheni za jeshi la Yemen na makundi ya muqawama wa Kiislamu katika eneo zitaendelea hadi mwisho wa uchokozi na kuondolewa mzingiro wa wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Wakati huo huo, Harakati ya Ukombozi wa Palestina (Popular Front for the Liberation of Palestine ) imepongeza hatua hiyo ya kishujaa ya wanajeshi wa Yemen. Imesema kuwa, mzingiro wa majini wa Bandari ya Haifa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni hatua muhimu inayoashiria mwanzo wa awamu mpya ya muqawama wa Yemen dhidi ya utawala wa Israel.

Haya yanajiri baada ya vikosi vya Yemen kuyatahadharisha mashirika ya ndege ya kimataifa juu ya kuanza tena safari za kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) huku operesheni za kulipiza kisasi za nchi hiyo ya Kiarabu zikiendelea.