Wakenya waendelea kujiunga na vita Ukraine licha ya maafa yanayowapa
Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya Wakenya wanaopigana katika vita vinavyoendelea huko Ukraine waliajiriwa kupitia maombi ya moja kwa moja na kampuni moja ya nchini Kenya, ambapo walitakiwa kurekodi video wakieleza nia yao ya kuajiriwa kama wanajeshi.
Haya yanajiri huku Mkuu wa Mawaziri wa Serikali ya Kenya, Musalia Mudavadi, akisema Ijumaa iliyopita kuwa, anapanga kufanya ziara ya kidiplomasia nchini Russia kama sehemu ya juhudi za kuwasaidia Wakenya waliokwama katika vita vya nchi hiyo na Ukraine au kunaswa katika vita hivyo.
Ushahidi unaonyesha kuwa, wengi kati ya walioomba kazi hiyo walikuwa maafisa wa zamani wa polisi na wanajeshi wastaafu, waliowasilisha waziwazi sifa zao za mafunzo ya kijeshi na kusema walikuwa tayari kupigana, wakitaka kazi ya kijeshi nje ya nchi.
Matokeo ya uchunguzi huo yanakadhibisha simulizi kwamba Wakenya waliokwama katika vita vya Ukraine hujikuta kwenye vita hivyo baada ya kudanganywa na maajenti.
Ushahidi unaonyesha kuwepo kwa njia iliyopangwa ya uajiri, ambapo mafunzo ya awali ya kiusalama hutolewa kama sifa ya kuajiriwa.
Video kadhaa zinaonyesha waombaji wakisisitiza uzoefu wao wa kutumia silaha, historia ya kushiriki katika operesheni za kijeshi na kusisitiza kwamba wako tayari kupelekwa vitani mara moja, huku wakikiri kuwa wanaelewa hatari za kushiriki katika mapigano ya moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Kenya, tangu 2022, shughuli za uajiri wa wapiganaji mamluki nchini Russia zimepanuka na kujumuisha mataifa mengine ya Afrika.
Baadhi ya ripoti zinasema karibu raia 1,400 kutoka bara la Afrika wanashiriki katika vita dhidi ya Ukraine.
Wizara ya Wizara ya Kigeni ya Kenya inakadiria kuwa zaidi ya Wakenya 200 huenda wamejiunga na jeshi la Russia kama mamluki.