Sudan yagundua makaburi ya halaiki yenye mamia ya miili Omdurman
Jeshi la Sudan limesema leo Alkhamisi kwamba, makaburi ya halaiki ya mamia ya raia yamegunduliwa katika mji wa Omdurman, kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.
Taarifa ya jeshi hilo imesema watu 648 walikuwa wamezuiliwa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ndani ya shule katika "hali ya kutisha na ya kinyama" katika kitongoji cha Salha huko Omdurman.
"Takriban watu 465 walipoteza maisha na kuzikwa katika makaburi ya halaiki, baadhi yao yalikuwa na zaidi ya miili 27," jeshi la Sudan limeeleza.
Hakukuwa na taarifa yoyote kutoka kwa kikundi hicho cha wanamgambo juu ya taarifa ya jeshi la Sudan kuhusu makaburi hayo ya umati.
Haya yanaripotiwa siku mbili baada ya Jeshi la Sudan (SAF) kutangaza kuwa, Jimbo la Khartoum limekombolewa kikamilifu na kwamba wapiganaji wote wa RSF wamefukuzwa mjini humo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Khartoum sasa imekuwa bila ya wanamgambo wa RSF kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka miwili.
Sudan imekumbwa na mzozo mbaya mno wa uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF tangu Aprili 2023.
Vita hivyo vimeshaua makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kukimbia makazi yao, ndani na nje ya Sudan.