RSF yashambulia tena kambi ya wakimbizi na kuua 14 Darfur, Sudan
Kwa akali watu 14 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi la mizinga la Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika jimbo la Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan.
Kamati ya Dharura ya Abu Shouk ilisema hayo jana Jumatano na kueleza kuwa, shambulio hilo lililenga kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk huko El-Fasher, mji mkuu wa jimbo hilo.
Kundi hilo la waasi halitajoa taarifa yoyote kufikia sasa juu ya tuhuma hizo za kufanya shambulio jipya la umwagaji damu huko huko Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan
El-Fasher imeshuhudia mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na RSF tangu Mei 2024, licha ya onyo la kimataifa kuhusu hatari ya ghasia katika mji huo ambao unatumika kama kitovu muhimu cha kibinadamu kwa majimbo matano ya Darfur.
Haya yanajiri siku moja baada ya serikali ya Sudan kutangaza kwamba, watu kadhaa wameuawa baada ya vikosi vya RSF kushambulia msafara wa misaada wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Al-Koma katika jimbo la Darfur Kaskazini.
Hii ni katika hali ambayo, idadi ya watu ambao wameikimbia Sudan tangu kuanza kwa vita vyake vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2023 ikipindukia milioni nne. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema hayo Jumanne na kuongeza kuwa, wengi wa walionusurika wanakabiliwa na makazi duni kutokana na uhaba wa fedha.
Vita hivyo vilivyoanza Aprili 2023, vimesababisha uharibifu mkubwa wa mali ya umma na miundombinu muhimu, kuua makumi ya maelfu ya watu, mbali na kulazimisha mamilioni kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.