Jeshi la Sudan latangaza kuukomboa kikamilifu mji wa Khartoum
Jeshi la Sudan (SAF) limetangaza kuwa Jimbo la Khartoum limekombolewa kikamilifu na kwamba wapiganaji wote wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) wamefukuzwa mjini humo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Khartoum imekuwa bila ya wanamgambo wa RSF kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka miwili.
Katika taarifa yake, Jeshi la Sudan, SAF limetangaza kwamba Khartoum imesafishwa kikamilifu na hakuna tena "waasi na wafuasi wao." SAF pia imeapa kuendelea na operesheni za kijeshi hadi maeneo yote yaliyoko chini ya udhibiti wa RSF yatakapokombolewa kikamilifu.
Katika taarifa nyingine tofauti, serikali ya Sudan ilisisitiza kuwa jeshi na washirika wake wataendelea na operesheni za kukomboa maeneo ambayo bado yanashikiliwa na RSF katika mikoa ya Kordofan na Darfur, magharibi mwa Sudan. "Tunatoa pongezi zetu kwa Wasudan wote kwa ukombozi kamili wa Jimbo la Khartoum, na tunawahakikishia watu wetu huko Kordofan na Darfur kwamba hakuna kitakachozuia njia yetu ya kuwafikia," imesema taarifa hiyo.
Sanjari na tangazo la kufukuzwa RSF kutoka Khartoum, jeshi la Sudan limetangaza kwamba wanamgambo wa RSF wamefukuzwa pia kwenye Jimbo la White Nile la kusini mwa mji mkuu, Khartoum. Wakati huo huo, mchambuzi mmoja wa masuala ya kijeshi wa Sudan Ahmed Ismail amesema kwamba kufanikiwa jeshi la Sudan kuyadhibiti majimbo ya Khartoum na White Nile ni ishara ya kuanza awamu mpya katika mzozo huo. Taarifa ya SAF imesema: "Jeshi linafaidika na ushindi wake unaoendelea tangu mapema 2025, wakati RSF inayumba kutokana na vikwazo vilivyoanzia katikati mwa Sudan na kumalizikia kupoteza udhibiti wa mji mkuu."
Sudan imekumbwa na mzozo mbaya mno wa uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF tangu Aprili 2023. Vita hivyo vimeshaua makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kukimbia makazi yao, ndani na nje ya Sudan.