Iran: Majigambo ya Trump kuhusu uharamia ni ‘kukiri wazi’ jinai
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138142-iran_majigambo_ya_trump_kuhusu_uharamia_ni_kukiri_wazi’_jinai
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imejibu kauli za Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye amejigamba kuwa Jeshi la Wanamaji la Marekani limetekeleza operesheni “kama maharamia” katika mzingiro wa baharini usio halali dhidi ya meli na bandari za Iran.
(last modified 2026-05-03T10:28:47+00:00 )
May 03, 2026 10:26 UTC
  •  Esmaeil Baghaei
    Esmaeil Baghaei

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imejibu kauli za Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye amejigamba kuwa Jeshi la Wanamaji la Marekani limetekeleza operesheni “kama maharamia” katika mzingiro wa baharini usio halali dhidi ya meli na bandari za Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, ameandika katika ujumbe kwenye mtandao wa X kwamba: “Rais wa Marekani ameelezea hadharani ukamataji wa kinyume cha sheria wa meli za Iran kuwa ni ‘uharamia,’ huku akijigamba waziwazi kwamba ‘tunatenda kama maharamia.’”

Baghaei ameongeza kuwa: “Hili halikuwa kosa la ulimi, bali lilikuwa kukiri kwa moja kwa moja na kwa uzito mkubwa tabia ya kijinai ya vitendo vyao dhidi ya usafiri wa kimataifa wa baharini.”

Aidha, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa: “Jumuiya ya kimataifa, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, lazima zipinge kwa uthabiti jaribio lolote la kuhalalisha ukiukaji huu wa wazi wa sheria za kimataifa.”

Trump alisema katika mkutano wa kisiasa huko Florida siku ya Ijumaa kwamba Jeshi la Wanamaji la Marekani limetekeleza operesheni “kama maharamia” alipokuwa akielezea operesheni ya kukamata meli za Iran.

Trump amesema: “Sisi … tulitua juu ya meli na tukaiteka. Tumechukua shehena za mizigo na mafuta. Hii ni biashara yenye faida kubwa sana. Sisi ni kama maharamia.”

Trump aliamuru mzingiro dhidi ya meli na bandari za Iran kuanzia tarehe 13 Aprili baada ya kutangaza usitishaji wa mapigano wa wiki mbili kufuatia vita vya kichokozi dhidi ya Iran vilivyodumu kwa siku 40.

Baada ya muda wa usitishaji huo kumalizika, alitangaza kuendelezwa kwa mzingiro huo, jambo ambalo limeelezwa kuwa ni ukiukaji wa masharti ya usitishaji vita.

Katika kipindi cha mzingiro huo, vikosi vya Marekani vimeripotiwa kukamata meli kadhaa za Iran, pamoja na shehena zake, wahudumu wa meli na hata familia zao.

Kwa hatua ya kujibu uharamia huo, Jamhuri ya Kiislamu, ambayo tayari ilikuwa imeufunga Mlango Bahari wa Hormuz kwa maadui na washirika wao, ilianza kuweka udhibiti mkali zaidi juu ya njia hiyo ya maji ya kimkakati.