Namna Marekani Ilivyokosa Kuwa na Mkakati Unaoeleweka Katika Kuamiliana na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138126-namna_marekani_ilivyokosa_kuwa_na_mkakati_unaoeleweka_katika_kuamiliana_na_iran
Naibu waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Wendy Sherman, amekosoa namna serikali ya Donald Trump inavyosimamia suala la vita dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, Washington haina mkakati unaoeleweka, wala mwenendo wa uchukuaji maamuzi ulioratibika, na kwamba mgogoro wa sasa hautatatuka pasi na kuirejea tena diplomasia.
(last modified 2026-05-02T17:45:10+00:00 )
May 02, 2026 17:20 UTC
  • Namna Marekani Ilivyokosa Kuwa na Mkakati Unaoeleweka Katika Kuamiliana na Iran

Naibu waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Wendy Sherman, amekosoa namna serikali ya Donald Trump inavyosimamia suala la vita dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, Washington haina mkakati unaoeleweka, wala mwenendo wa uchukuaji maamuzi ulioratibika, na kwamba mgogoro wa sasa hautatatuka pasi na kuirejea tena diplomasia.

Sherman alikuwa kwa miaka kadhaa mjumbe wa timu ya Marekani katika mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mazungumzo ambayo hatimaye yalipelekea kutiwa saini mwaka 2015 mkataba wa makubaliano ya nyuklia yaliyojulikana kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA); makubaliano ambayo Trump aliyataja kuwa ndiyo mabaya zaidi kuwahi kusainiwa na Marekani katika historia yake; na kutokana na mashinikizo ya Netanyahu na lobi ya Uzayuni, wakati alipoingia madarakani katika muhula wake wa kwanza wa urais mwaka 2018 alichukua hatua ya kuiondoa nchi hiyo kwenye makubaliano hayo.
Hivi sasa akthari ya wanafikra nchini Marekani na barani Ulaya wanakiri kuwa, mkataba wa JCPOA yalikuwa makubaliano bora kabisa kwa ajili ya ukaguzi na usimamizi wa mpango wa nyuklia wa Iran. Lau kama makubaliano ya JCPOA yangeendelea kudumu, eneo la Asia Magharibi lisingekumbwa na mabalaa yote haya yanayoshuhudiwa ya migogoro, kuvurugika kwa utulivu na jinai chungu nzima za kinyama zinazofanywa na Wazayuni na Marekani. Kisingizio kikubwa zaidi walichotumia Trump na Netanyahu kuanzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran ni mpango wa amani wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu. Bila shaka mpango huo wa nyuklia wa Iran ni kisingizio tu kilichotolewa kuhalalisha uadui na mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, lakini lengo lao hasa ni kuuangusha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuigawanya Iran vipande vipande.
Hata hivyo, jibu la mshtukizo la Iran kwa uchokozi huo na vipigo vya kushangaza ilivyotoa vya kuvitwanga vituo vyote vya Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi vimebadilisha milingano ya nguvu za kisiasa na kiusalama ya eneo hili. 
Inavyompitikia Trump akilini mwake hivi sasa ni kwamba kwa kuiwekea Iran mzingiro wa baharini na mashinikizo ya kiuchumi, sambamba na kutoa vitisho vya mashambulizi, ataweza kukipata kile alichoshindwa kukitia mkononi kupitia vita vya siku 40. Ili kuzipa uhalali hatua zake za kihalifu na kichokozi Trump amekuwa akirudia kila mara dai lake kwamba eti hataki Iran iwe na silaha za nyuklia. Hii ni pamoja na kuwa, Iran haijawahi katu kufuatilia uundaji na umiliki wa silaha za nyuklia; na hadi kabla Marekani haijajitoa kwenye makubaliano ya JCPOA, shughuli zake zote za nyuklia zilikuwa chini ya uangalizi na ukaguzi mkali zaidi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA.

Wendy Sherman, wanasiasa na wananadharia wengine wengi mashuhuri wa Marekani, kama vile John Mearsheimer na Richard Haas, ambao wana utambuzi na uzoefu wa kufanya majadiliano na mazungumzo na Wairan, wanaitakidi kuwa shambulio aliloanzisha Trump dhidi ya Iran limeshindwa na limeibebesha Marekani mzigo mkubwa wa gharama, na wangali wanasisitiza kuwa diplomasia ndio njia bora zaidi kwa Marekani kujinasua kwenye mkwamo wa mgogoro huo. 
Wendy Sherman, ameashiria matamshi ya waziri wa vita wa Marekani, Pete Hegseth aliyedai kwamba Washington imefanikiwa katika operesheni za kijeshi dhidi ya Iran na kusema: "Hegseth anasema jeshi limefanya kazi nzuri ya kipekee na limefikia malengo yake, lakini katika uhalisia, hivi sasa kuna mkwamo kati ya Iran kuudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz na mzingiro wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran".
Naibu waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani amesisitiza kwamba, yeye hadhani kama shambulizi jipya la Marekani dhidi ya Iran litaweza kubadilisha mahesabu ya Tehran au kuondoa mkwamo uliopo. Sherman amelinganisha hali ya sasa na ya kipindi cha mazungumzo ya JCPOA na kueleza kwamba: "Wakati wa mazungumzo ya JCPOA, Marekani ilikuwa na wafanyamazungumzo na wataalamu wazuri, na mwenendo wa uchukuaji maamuzi ulikuwa wa kimantiki, lakini sivyo ilivyo hivi sasa chini ya utawala wa Trump".
Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa serikali ya zamani ya Marekani amekosoa pia muelekeo wa utawala wa Trump wa kujaribu kuipigisha magoti Iran, akisema: "Trump anadhani anaweza kila mara kuiadhibu Iran na kwamba mwishowe Marekani itaweza kuonyesha uhimilivu zaidi kuliko Iran, lakini kama walivyoeleza wachambuzi wengi, dhana hii sio sahihi".
Katika kipindi cha usitishaji vita na wakati wa duru moja ya mazungumzo iliyofanyika kati ya Marekani na Iran mjini Islamabad, Trump ameendelea kuitaka Iran isalimu amri kikamilifu. Shakhsia kama vile Wendy Sherman, John Mearsheimer, na Richard Haas wamesisitiza mara kadhaa kwamba, kusalimu amri Iran mbele ya Marekani si chochote zaidi ya njozi na udhanifu tu.
Nukta kuu ya ukosoaji wa Wendy Sherman, wanasiasa na wachambuzi wengine ndani ya Marekani wanaomkosoa Trump ni kwamba, vita visivyo na mkakati unaoeleweka, uchukuaji maamuzi wa kimihemko, kutokuwa na elimu ya kuitambua Iran, na kung’ang’ania kutoa masharti ya udhalilishaji katika mazungumzo kunaonyesha kuwa, Marekani sio tu haijayakaribia malengo yake, lakini pia imenasa kwenye mkwamo ambao njia pekee ya kujinasua nao ni kurejea haraka kwenye diplomasia, inayozingatia uhalisia na kukubali hatua za upande wa pili za kupunguza mivutano. Ili kujenga hali ya kuaminiana ya kufanyia mazungumzo na kufikia makubaliano, Iran kwa upande wake, inataka kwanza vita vikomeshwe kikamilifu na kuwepo suluhu endelevu.../