IRGC: Hakuna dola linaloweza kudhoofisha azma ya taifa la Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138144-irgc_hakuna_dola_linaloweza_kudhoofisha_azma_ya_taifa_la_iran
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limelishukuru taifa la Iran kwa kusimama kidete kuilinda nchi na msimamo wake imara wa Kiislamu kupitia maandamano ya kuonyesha umoja na mshikamano nchini.
(last modified 2026-05-03T10:42:06+00:00 )
May 03, 2026 10:25 UTC
  • Maandamano ya hamasa ya wananchi wa Iran kumuunga mkono Ayatullah Mojtaba Khamenei
    Maandamano ya hamasa ya wananchi wa Iran kumuunga mkono Ayatullah Mojtaba Khamenei

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limelishukuru taifa la Iran kwa kusimama kidete kuilinda nchi na msimamo wake imara wa Kiislamu kupitia maandamano ya kuonyesha umoja na mshikamano nchini.

Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, jeshi hilo liliashiria mikusanyiko mikubwa ya nchi nzima, hususan ile iliyofanyika hivi majuzi katika kumbukumbu ya kuzaliwa Imamu wa Nane wa Waislamu katika kizazi cha Mtume Muhammad (SAW), Imam Reza (AS), na kampeni ya wananchi wa Iran ya kuihami na kuilinda nchi inayojulikana kwa jina la (Janfada-e-Iran) ambayo imeshuhudia mamilioni ya watu wakijiandikisha na kutangaza kuwa wako tayari kusabilia maisha yao ili kuilinda na kuihami Iran dhidi ya maadui.

Taarifa ya IRGC kwa wananchi imeeleza kuwa: "Iran na watu wake kamwe hawatapiga magoti na kusalimu amri mbele ya maadui zao, na hakuna nguvu inayoweza kudhoofisha azma hiyo.

Jeshi la IRGC limepongeza mikusanyiko ya hamasa ya  wananchi wa Iran na kuitaja kuwa "haina kifani", na kueleza namna maandamano hayo yalivyoendelea katika kipindi chote cha siku 40 za mashambulizi ya Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na hadi leo ambapo wananchi wa Iran wanaendelea kukusanyika katika medani na maeneo mbalimbali ya nchi.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limetaja ushiriki huo wa hamas wa wananchi kote nchini kuwa ni kielelezo cha utiifu kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, ambaye amechaguliwa kuchukua nafasi ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi aliyeuawa shahidi mwanzoni mwa vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.