Kwa nini Uhispania imeongeza mashinikizo dhidi ya Israel?
Bunge la Uhispania limepitisha muswada unaoitaka serikali ya nchi hiyo kuacha kuuzia utawala ghasibu wa Israel zana zozote za kijeshi.
Mpango huo, uliowasilishwa na muungano wa mrengo wa kushoto wa Somar, pamoja na vyama vya upinzani vya Podemos na Catalan Republican Left (ERC), ulikabiliwa na upinzani kutoka kwa chama cha wahafidhina cha People's Party (PP) na chama cha mrengo wa kulia cha VOX, lakini hatimaye ukaidhinishwa kwa kura 176 dhidi ya 171. Mpango huo unatoa wito wa kupigwa marufuku usafirishaji wa zana za kijeshi, zikiwemo helmeti, vizibao vya kuzuia risasi, mafuta yenye matumizi ya kijeshi kwa utawala wa Israel, pamoja na kuzifanyia marekebisho sheria za biashara za nje ili kuzuia mikataba ya kijeshi na tawala zinazotuhumiwa kuhusika na mauaji ya halaiki au jinai dhidi ya binadamu.
Huko nyuma Wizara ya Ulinzi ya Uhispania ilitangaza kwamba mikataba yote ya ununuzi wa silaha kutoka kwa utawala wa Israel ilisitishwa kuanzia tarehe 7 Oktoba 2023, isipokuwa ile inayohusiana na ukarabati na matengenezo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania aidha amesema nchi hiyo imeacha kuuzia silaha utawala wa Israel tangu kuanza vita huko Gaza. Wizara hiyo ilitoa taarifa hiyo kujibu barua rasmi iliyotumwa na mawaziri kutoka chama cha muungano cha mrengo wa kushoto cha Uhispania, Somar. Chama hicho kilikuwa kimetoa wito kwa washirika wake katika serikali kutekeleza kikamilifu vikwazo vya silaha dhidi ya Israel.
Uhispania ni mkosoaji mkubwa wa vitendo vya jinai vya Israel katika vita vya Gaza hususan mauaji ya halaiki na matumizi ya njaa kama silaha dhidi ya Wapalestina. Viongozi wa vyama vya mrengo wa kushoto nchini Uhispania wamekuwa wakikariri ukosoaji wao mkali dhidi ya Israel. Mmoja wa viongozi hao wa chama cha Podemos, Iván Bellara, amemtaja Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel, kuwa "Hitler wa Zama" baada ya bunge la Uhispania kupitisha mswada wa kupiga marufuku uuzaji wa silaha kwa Israel na kulitaka baraza la mawaziri la nchi hiyo kufanya mkutano wa dharura wiki hii na kutoa amri rasmi ya kupiga marufuku uuzaji wa silaha kwa utawala huo.

Pedro Sanchez, Waziri Mkuu wa Uhispania pia amekuwa akiukosoa mara kwa mara utawala wa Kizayuni. Katika hotuba yake mjini Davos, Uswisi, Januari mwaka jana, alionya, akizungumzia mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, kwamba usalama na utulivu wa Asia Magharibi uko hatarini na kwamba mashambulizi ya kinyama ya utawala huo yanahatarisha mifumo ya kijamii ya pande kadhaa katika eneo. Sanchez aliandika hivi karibuni kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Israel ni utawala wa mauaji ya halaiki na tuna haki ya kutokuwa na uhusiano wa kibiashara na utawala kama huo."
Viongozi wengine waandamizi wa Uhispania pia wamechukua misimamo muhimu kuhusiana na vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni. Miongoni mwao ni Ion Bilara, Waziri wa Haki za Kijamii wa Uhispania, ambaye amesema: "Israel imeacha mamia ya maelfu ya watu (huko Gaza) bila umeme, maji wala chakula, na inawashambulia raia kwa mabomu, ambayo ni adhabu ya pamoja na ukiukwaji hatari wa sheria za kimataifa. Jambo hilo linaweza kuchukuliwa kuwa ni uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari."
Ingawa Uhispania inachukuliwa kuwa miongoni mwa nchi za Ulaya zinazoukosoa vikali utawala wa Kizayuni na kuunga mkono haki za Wapalestina, lakini misimamo ya nchi nyingine za Ulaya kuhusu vita vya Gaza na kuendelea mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya watu wa ukanda huo kunaonyesha mgawanyiko wa wazi uliopo kati ya nchi hizo kuhusu suala hilo. Baadhi ya nchi za Ulaya kama Uhispania, Ireland, Ubelgiji na Norway zimetoa wito hadharani wa kutambuliwa taifa la Palestina na zimechukua msimamo wa kulaani vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza. Hii ni katika hali ambayo washirika wa karibu wa Marekani barani Ulaya kama vile Ujerumani na Austria na nchi za Ulaya Mashariki kama Jamhuri ya Czech na Hungary wamechukua misimamo ya kuiunga mkono Israel na kuendelea operesheni za kijeshi za utawala huo wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza pamoja na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina kwa kisingizio cha kujilinda. Ujerumani ni nchi ya pili kwa mauzo ya silaha kwa utawala wa Israel baada ya Marekani.
Msimamo unaochukuliwa na baadhi ya nchi za Ulaya mfano wa Uhispania dhidi ya Israel kwa kulaani mauaji ya halaiki na utumiaji njaa kama silaha na wakati huo huo kuzuia kutumwa misaada ya kibinadamu na utawala wa Kizayuni unaolenga kuwaangamiza watu wa Gaza na kuwalazimisha kuondoka Gaza, ni mambo yanayothibitisha wazi kuwa zama za uungaji mkono wa pande zote kwa Israel, hata miongoni mwa nchi za Ulaya, zimeisha. Tel Aviv bila shaka inaendelea kupoteza nguvu laini na uwezo wake wa kuathiri maoni ya umma katika nchi za Magharibi hasa za Ulaya na Marekani katika kuhalalisha vitendo vyake vya jinai dhidi ya watu madhlumu wa Gaza. Wakati huo huo jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza ziko wazi na hazifichiki kiasi kwamba hata nchi za Ulaya mfano wa Uhispania zimechukua msimamo na hatua za kivitendo za kushadidisha mashinikizo dhidi ya Tel Aviv.