Pezeshkian: Marekani inafanya uporaji mchana kweupe
Rais Masoud Pezeshkian amesema kuwa, rais wa Marekani Donal Trump alisema akiwa nchini Saudia kwamba watu wengine wanapora na kuiba wakati mwenyewe Trump ndiye anayefanya wizi na uporaji mchana kweupe na mbele ya macho ya walimwengu.
Rais Pezeshkian amesema hayo Bungeni wakati wa kumbukumbu za kumuenzi Rais Ibrahim Raisi, Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Iran, Amir-Abdollahian pamoja na viongozi wengine kadhaa wa ngazi za juu waliokufa shahidi kwenye ajali ya helikopta mwaka mmoja uliopita na kuongeza kuwa: Kitu kilichonigusia sana wakati nilipotembelea familia za mashahidi hao wa kuhudumia taifa, ni jinsi maisha yao yalivyokuwa ya chini kabisa. Nyumba ya mama yake shahid Raisi ni ya maisha ya chini kuliko maelezo. Hata nyumba yake hapa Tehran, ni nyumba iliyoko katika sehemu ya kawaida kabisa ya mji. Mashahidi wengine nao waliishi maisha ya chini kabisa.
Rais Pezeshkian aidha amesema: "Wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanapaswa kwenda kwenye nyumba za wapendwa wetu hawa wakaone jinsi maisha yao yalivyokuwa ya chini mno. Usafi wa imani, uaminifu na uzuhdi huzungumza zaidi kuliko maneno, kashfa na majigambo yote."
Vilevile amesema: "Licha ya kuweko njama nyingi, lakini wapendwa wetu hawa walijitolea kwa kila kitu, wananchi wakawakubali. Kwa kweli hakuna kinachoweza kufikia thamani ya kazi yao kubwa."
Amesema: "Hayo ndiyo maisha ya viongozi wetu hao wapendwa, lakini utasikia baadhi ya watu wanasema mambo ambayo yanakufanya uone haya kuyasema. Trump alisema huko Saudi Arabia kwamba eti viongozi hao wa Iran walikuwa wanapora na kuiba kila kitu, (kinyume kabisa na ukweli wa mambo). Kwa kweli tunayemuona akifanya wizi na uporaji mchana kweupe na mbele ya macho ya walimwengu ni Trump mwenyewe."