Hamas yapongeza mataifa 80 kwa kulaani jinai za Israel huko Gaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imekaribisha kwa mikono miwili taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi 80 duniani, zikisisitiza kwamba Gaza inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu tangu kuanza kwa vita vya Israel Oktoba 7 mwaka 2023.
Katika taarifa, Hamas imeponeza msimamo wa pamoja wa nchi 80 duniani, ikisisitiza kwamba Ukanda wa Gaza unakabiliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu kufuatia uvamizi wa Israel tangu Oktoba 7, 2023.
Hamas imesisitiza kuwa: Msimamo huu unasisitiza kupanuka kwa wigo wa upinzani wa kimataifa dhidi ya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanya wanajeshi makatili wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
"Taarifa iliyotolewa na nchi hizo 80 inatumika kama shinikizo kubwa la kutoa misaada ya kibinadamu kwa taifa la Palestina, kukomesha uhalifu wa njaa, na kuvunja mzingiro wa kikatili uliowekwa juu ya Gaza," Hamas imeeleza.
Haya yanajiri huku wataalamu wa usalama wa chakula wakionya kuwa, Gaza inakabiliwa na baa la njaa iwapo mzingiro huo hautaondolewa, huku mashirika ya misaada yakiripoti kuwa yalimaliza akiba ya chakula wiki chache zilizopita. Takriban wakazi wote milioni 2.3 wa Gaza wanategemea chakula cha msaada.
Haya yanajiri huku utawala ghasibu wa Israel ukiendelea kufanya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza. Zaidi ya Wapalestina 50 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya punde zaidi ya anga ya Israel kwenye jengo la makazi, kaskazini mwa Gaza.
Wizara ya Afya ya Gaza imesema watoto na wazee 29 waliofariki dunia katika siku za hivi karibuni Gaza wamewekwa katika orodha ya "vifo vinavyotokana na njaa", na maelfu zaidi wako hatarini kufa njaa.