Jenerali Baqeri: Vikosi vya Iran havitasita kujibu vitisho vya maadui
(last modified Fri, 23 May 2025 06:26:52 GMT )
May 23, 2025 06:26 UTC
  • Jenerali Baqeri: Vikosi vya Iran havitasita kujibu vitisho vya maadui

Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Iran amesema wanajeshi wa nchi hii hivi sasa wanatengeneza aina mbalimbali za ndege zisizo na rubani na ndege ndogo, akionya kwamba Jamhuri ya Kiislamu itajibu vitisho vyovyote vya maadui kwa jibu lenye mlingano sawa.

Akizungumza baada ya ziara ya ukaguzi wa mipaka ya kusini mashariki na mashariki ya nchi jana Alkhamisi, Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesisitiza kwamba, lengo kuu la Iran ni kuimarisha uwezo wake wa kuzuia hujuma, ulinzi thabiti, usalama wa kudumu, na utulivu wa kikanda.

Amebainisha kuwa, vikosi vya jeshi la Iran haswa Vikosi vya Ardhini vya nchi hii, vimepiga hatua kubwa ya kimkakati kwa kuunda teknolojia ya hali ya juu na mifumo ya ulinzi ya hali ya juu inayoendana na hali halisi ya ulimwengu.

"Mojawapo ya mafanikio muhimu ya kijeshi ya Iran," Baqeri amesema, "ni uundaji wa ndege ndogo zilizozalishwa kwa shabaha ya kukabiliana na ndege zisizo na rubani za adui."

Meja Jenerali Baqeri  ameonya kuwa, shambulio lolote dhidi ya Iran, litawasababishia hasara kubwa wavamizi na wala hawataweza kuambulia chochote.

Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitavumilia uchokozi dhidi ya ardhi yake na haitacha uvamizi upite bila kujibiwa.

Meja Jenerali Baqeri pia ameashiria juhudi zilizoratibiwa kati ya Jeshi na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika kulinda usalama wa taifa na kuongeza kuwa, vikosi vyote vya majeshi vinafanya kazi kwa ushirikiano na IRGC ili kudumisha usalama wa ndani na wa kikanda inapohitajika.