Pigo kwa wanajeshi vamizi wa Israel mashariki mwa Khan Yunis
Wanamapambano wa kambi ya Muqawama wa Kiislamu huko Khan Yunis katika Ukanda wa Ghaza, wameendelea kuwatia hasa wanajeshi vamizi wa utawala wa Kizayuni. Wanajeshi zaidi wa Israel wanaendelea kuripukiwa na mabomu na kupigwa risasi na vifaa vyao vya kijeshi kushambuliwa na wamamapambano wa Palestina.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Fars, Saraya al-Quds (tawi la kijeshi la harakati ya Jihadul Islami ya Palestina) lilitangaza jana Alkhamisi kwamba wamefanikiwa kulinasa kundi la wahandisi wa jeshi la Israel katika mtego wao wa miripuko na kuwaripulia mbali. Saraya al-Quds imeongeza kuwa, wanamapambano wao wamefanikiwa kuwarubuni wanajeshi hao mashariki mwa mji wa Khan Yunis na kuwalazimisha kuingia kwenye nyumba ambayo tayari ilikuwa imetegwa mabomu na baadaye kuiripua nyumba hiyo mara baada ya wanajeshi wa Israel kujiingiza ndani ya nyumba hiyo.
Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina aidha imesema katika taarifa yake kwamba, mara baada ya vikosi vya Muqawama kuwarubuni wanajeshi vamizi wa Israel kuingia ndani ya nyumba hiyo wamewashambulia na kuripua nyumba hiyo na kulazimisha helikopta za utawala wa Kizayuni kupelekwa haraka katika eneo hilo kwa ajili ya kusafirisha maiti na majeruhi wa Kizayuni na kuficha taarifa za kipigo hicho zisiwafikie walimwengu. Tarehe 19 mwezi huu wa Mei, utawala wa Israel uliwataka wakaazi wa maeneo makubwa ya Khan Yunis, Bani Suhayla na Abbasan waondoke kwenye maeneo yao na kuhamia upande wa magharibi katika eneo la Al-Mawasi. Wazayuni pia wamewatishia wakazi wa maeneo hayo na kudai kuwa watafanya mashambulizi ya kikatili mno ambayo hawajawahi kuyafanya katika eneo hilo kwa madai ya eti kuharibu uwezo wa muqawama. Lakini pamoja na jinai zote hizo za Wazayuni, bado wanamapambano wa Palesitna wako kwenye mistari ya mbele ya mapambano na wanaendelea kuwasababishia maafa wanajeshi vamizi wa Israel.