Kamanda wa al-Shabaab ni miongoni mwa magaidi 45 walioangamizwa Somalia
Vikosi vya usalama vya Somalia vimeangamiza magaidi 45 wa al-Shabaab, ikiwa ni pamoja na mkuu wa genge hilo aliyehusika na mashambulizi ya mara kwa mara ya mabomu mjini Mogadishu tangu 2023.
Taarifa ya Shirika la Taifa la Ujasusi na Usalama la Somalia (NISA) imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa magaidi hao wameangamizwa kwenye operesheni kabambe zilizofanyika katika mikoa ya Hiran na Shabelle ya Chini.
Shirika hilo limesema, mashambulizi sita ya anga yamefanyika katika eneo la El-Hareeri huko Hiran kuanzia Jumanne mchana hadi mapema jana Jumatano, na kuua wale waliotajwa na taarifa hiyo kuwa ni: "wapiganaji 45 wa Khawarij, wakiwemo viongozi na wanamgambo."
Serikali ya Somalia inaliitaja kwa jina la Khawarij; genge la kigaidi la al-Shabaab ambalo limejitangaza kuwa tawi la mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Ahmed Mohamud, afisa wa usalama katika eneo hilo amesema kuwa, idara za ujasusi zilitumia ndege zisizo na rubani kupiga eneo ambalo genge hilo na maafisa wake wakuu walikuwa wamejificha.
Kwa mujibu wa NISA, waliouawa katika operesheni hizo ni pamoja na kiongozi mkuu wa al-Shabaab ambaye anahusika na mashambulizi ya mabomu mjini Mogadishu tangu 2023. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kiongozi huyo wa al-Shabab ameangamizwa kwenye operesheni iliyofanyika karibu na Sabib katika eneo la Shabelle ya Chini.
Somalia imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama kwa muda mrefu, huku magenge ya kigaidi ya al-Shabaab na Daesh (ISIS) yakiwa tishio zaidi la usalama. Al-Shabaab wamekuwa wakipigana na serikali ya Somalia kwa zaidi ya miaka 16 na wamefanya jinai kubwa nchini Somalia na nje ya nchi hiyo.