Mbunge wa US ataka Gaza iangamizwe kwa nyuklia kama Hiroshima
(last modified Fri, 23 May 2025 11:55:18 GMT )
May 23, 2025 11:55 UTC
  • Mbunge wa US ataka Gaza iangamizwe kwa nyuklia kama Hiroshima

Mbunge wa jimbo la Florida wa chama cha Republican, Randy Fine ameashiria shambulio la bomu la nyuklia la Marekani dhidi ya Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kutoa wito wa kuangamizwa Gaza kwa silaha za nyuklia.

Katika mahojiano na Fox News jana Alkhamisi, Fine alilinganisha vita vinavyoendelea vya Israel na mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia na kueleza kuwa, mashambulizi ya mabomu ya nyuklia huko Hiroshima na Nagasaki yalisababisha "kujisalimisha bila masharti" na kwamba "hatua sawa" inapaswa kufanyika Gaza.

"Katika Vita vya Pili vya Dunia, hatukufanya mazungumzo ya kujisalimisha kwa Wanazi, hatukufanya mazungumzo ya kujisalimisha na Wajapan. Tuliwapiga (kwa silaha za) nyuklia Wajapan mara mbili ili kupata kujisalimisha bila masharti. Hiyo inahitaji kuwa sawa hapa (Gaza)," amesema.

Hapo awali Fine alikosolewa kwa matamshi yake kuhusu vita hivyo vya Wazayuni dhidi ya Gaza, ambapo Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR) liliyaeleza matamshi hayo kuwa "yamejaa chuki dhidi ya Waislamu, Wamarekani na Wapalestina."

Mbunge wa jimbo la Florida wa chama cha Republican, Randy Fine

CAIR, shirika kubwa zaidi la kutetea haki za kiraia na utetezi wa Waislamu nchini Marekani, jana Alkhamisi ililaani vikali kauli ya hivi punde zaidi ya Fine na kuwataka viongozi wa Republican na Democratic kuchukua hatua za haraka kukemea hadharani matamshi hayo ya kushajiisha mauaji ya halaiki; na kumuondoa katika kamati na vikao vyote vya bunge.

CAIR ilisema kauli ya Fine ni uchochezi wa wazi wa ghasia, inayohatarisha usalama wa Waislamu wa Marekani na Wapalestina, kwa kutoa wito wa mauaji ya kimbari ya nyuklia dhidi ya zaidi ya Wapalestina milioni mbili wa Gaza, ambapo nusu yao ni watoto.