Utawala wa Kizayuni waendelea kukodolea macho ya tamaa ardhi ya Somalia
(last modified Thu, 21 Nov 2024 03:47:59 GMT )
Nov 21, 2024 03:47 UTC
  • Utawala wa Kizayuni waendelea kukodolea macho ya tamaa ardhi ya Somalia

Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendeleza njama zake za kutaka kuwa na kituo cha kijeshi kaskazini mwa Somalia, kupitia eneo lililojitangazia uhuru wake la Somaliland, suala ambalo linaleta uwezekano mkubwa wa kuongezeka hatari za kiusalama baina ya nchi za ukanda huo.

Kwa mujibu wa Middle East Eye, utawala wa Kizayuni unakodolea macho ya tamaa eneo la kaskazini mwa Somalia kwa shabaha ya kuwa na kituo cha kijeshi kitakachokuwa kinaangalia kwa karibu safari za baharini za Lango Bahari la Bab al Mandab la nchini Yemen.

Katika mkabala wa suala hilo, utawala wa Kizayuni unapanga kuitambua rasmi Somaliland kuwa ni nchi licha ya sheria zote za kimataifa kuonesha kuwa hilo ni eneo ambalo haliwezi kutenganishwa na maeneo mengine ya Somalia.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa njama za kuweka mikataba na kujaribu kutambua uhuru wa Somaliland zinahatarisha usalama wa nchi za eneo hilo zima lakini pia huenda ni katika njama za Wazayuni za kuilazimisha Somalia itambue uwepo wa dola pandikizi la Israel.