WHO: Virusi vya Hanta si sawa na vya COVID-19
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138264-who_virusi_vya_hanta_si_sawa_na_vya_covid_19
Kufuatia mlipuko wa virusi vya Hanta au kwa kiingereza Hantavirus kuzua taharuki miongoni mwa umma kufuatia vifo vya watu watatu na wengine kadhaa wanapata matibabu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limesisitiza kuwa mlipuko wa virusi huo kutoka meli ya kifahari ya kitalii ya MV Hondius si sawa na wa virusi vya COVID-19 na kwamba hatari ya virusi hivyo kuenea kwa jamii kwa ujumla bado ni ndogo sana.
(last modified 2026-05-09T09:43:50+00:00 )
May 09, 2026 09:39 UTC
  • WHO: Virusi vya Hanta si sawa na vya COVID-19

Kufuatia mlipuko wa virusi vya Hanta au kwa kiingereza Hantavirus kuzua taharuki miongoni mwa umma kufuatia vifo vya watu watatu na wengine kadhaa wanapata matibabu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limesisitiza kuwa mlipuko wa virusi huo kutoka meli ya kifahari ya kitalii ya MV Hondius si sawa na wa virusi vya COVID-19 na kwamba hatari ya virusi hivyo kuenea kwa jamii kwa ujumla bado ni ndogo sana.

Kauli hiyo imetolewa Ijumaa mjini Geneva Uswisi na msemaji wa WHO, Christian Lindmeier wakati shirika hilo linaendelea kuratibu hatua za kukabiliana na mlipuko huo uliotokea katika meli iliyolazimika kutia nanga nchini Cabo Verde kuchukua hatua za kitababu na sasa inakaribia visiwa vya Canary barani Ulaya.

Kwa mujibu wa WHO, watu wanane wameambukizwa hadi sasa, wakiwemo watu watatu waliopoteza maisha, huku wagonjwa watano wakithibitishwa na maabara kuwa na maambukizi vya ya aina nadra ya virusi vya Andes vinavyopatikana Argentina.

Msemaji huyo amesema, “hata baadhi ya watu waliokuwa kwenye vyumba pamoja ndani ya meli hiyo hawakuambukizana, jambo linaloonesha kuwa virusi hivyo haviambukizwi kwa urahisi kama ilivyokuwa kwa COVID-19.”

WHO imefafanua kuwa virusi vya Hanta husambazwa zaidi kupitia mawasiliano ya karibu na ya muda mrefu na mtu aliyeambukizwa, hasa kwa wanafamilia, wapenzi au wahudumu wa afya.

Aidha, WHO imesema mhudumu wa ndege kutoka Uholanzi aliyewahi kuwasiliana kwa muda mfupi na mmoja wa wagonjwa waliokufa alipimwa na kukutwa hana maambukizi ya virusi hivyo.

Shirika hilo limesema tukio hilo linaonesha wazi kuwa hatari ya maambukizi kwa umma wa kawaida bado iko chini sana.

Kwa mujibu wa taarifa za WHO, mgonjwa wa kwanza alianza kuonesha dalili tarehe 6 Aprili 2026 kabla ya kufariki akiwa ndani ya meli hiyo.

WHO imeeleza kuwa hakuna abiria wala wafanyakazi waliobaki ndani ya meli wanaoonesha dalili za virusi hivyo kwa sasa.

Shirika hilo linaendelea kufuatilia watu wote waliowahi kuwasiliana na wagonjwa hao kupitia orodha za wasafiri wa ndege, meli na maeneo mbalimbali yaliyotembelewa.