Vikosi vya Iran vyashambulia meli za kivita za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138240-vikosi_vya_iran_vyashambulia_meli_za_kivita_za_marekani
Msemaji wa Kamandi ya Khatam alAnbiya ya Majeshi ya Iran amesema kwamba vikosi vya Iran vimetoa jibu la papo hapo na lenye nguvu kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani katika eneo muhimu la MlangoBahari wa Hormuz pamoja na ukanda wa pwani wa kusini mwa Iran.
(last modified 2026-05-08T11:22:11+00:00 )
May 08, 2026 11:20 UTC
  • Vikosi vya Iran vyashambulia meli za  kivita za Marekani

Msemaji wa Kamandi ya Khatam alAnbiya ya Majeshi ya Iran amesema kwamba vikosi vya Iran vimetoa jibu la papo hapo na lenye nguvu kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani katika eneo muhimu la MlangoBahari wa Hormuz pamoja na ukanda wa pwani wa kusini mwa Iran.

Katika taarifa yake, Kanali Ebrahim Zolfaghari amesema jeshi “la kichokozi, la kigaidi na lisiloheshimu sheria la Marekani, Alhamisi limevunja makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kulenga meli ya mafuta ya Iran.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, meli hiyo ya mafuta ilikuwa ikisafiri kutoka maji ya pwani ya Iran katika eneo la Jask, ikielekea MlangoBahari wa Hormuz wakati iliposhambuliwa.

Katika tukio jingine lililotokea karibu wakati huohuo, meli nyingine ya Iran iliripotiwa kushambuliwa ilipokuwa ikiingia katika MlangoBahari wa Hormuz, mkabala na bandari ya Fujairah katika Falme za Kiarabu (UAE).

Msemaji huyo aliongeza kuwa sambamba na matukio hayo, vikosi vya Marekani, vikishirikiana na baadhi ya nchi za eneo hilo, vilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya kiraia katika majimbo ya pwani.

Mashambulizi hayo ya angani yaliripotiwa kulenga maeneo ya Bandar Khamir, Sirik, na Kisiwa cha Qeshm.

Kwa mujibu wa taarifa ya kijeshi, jibu la Majeshi ya Iran lilikuwa la haraka na la maamuzi.

Vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilianzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya meli za kijeshi za Marekani mashariki mwa MlangoBahari wa Hormuz na kusini mwa bandari ya Bandar Chabahar. 

Taarifa zimebaini kuwa operesheni hiyo ya Iran ilisababisha uharibifu mkubwa kwa baadhi ya manowari za Marekani.

Aidha Kanali Ebrahim Zolfaghari ameonya kuwa Marekani na washirika wake wanapaswa kutambua kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa majibu makali na ya haraka kwa kitendo chochote cha uchokozi au uvunjaji wa mipaka, kama ambavyo imefanya hapo awali.