Wapinzani Afrika Kusini waapa kumuondoa madarakani Ramaphosa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138260-wapinzani_afrika_kusini_waapa_kumuondoa_madarakani_ramaphosa
Julius Malema, kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) nchini Afrika Kusini, amemtaka Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo ajiuzulu haraka iwezekanavyo na taratibu za kumfungulia mashtaka zianze.
(last modified 2026-05-09T09:56:39+00:00 )
May 09, 2026 09:54 UTC
  • Chama cha EFF chamtaka Ramaphosa ajiuzulu
    Chama cha EFF chamtaka Ramaphosa ajiuzulu

Julius Malema, kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) nchini Afrika Kusini, amemtaka Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo ajiuzulu haraka iwezekanavyo na taratibu za kumfungulia mashtaka zianze.

Chama cha EFF kinachoongozwa na Malema ni kati ya vyama vya upinzani vilivyopeleka suala hilo mahakamani, vikiwatuhumu wabunge wa chama tawala ANC kwa kutumia wingi wao wa viti vya bunge kumlinda Ramaphosa mkabala wa kuwajibishwa.

Mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini jana Ijumaa ilianza kusikiliza tena kesi ya mashtaka dhidi ya Rais Cyril Ramaphosa kuhusu ya kashfa ya kupatikana kiasi kikubwa cha fedha za kigeni ndani ya sofa katika nyumba yake ya shambani mwaka 2020.

Mkuu wa zamani wa ujasusi aliwasilisha malalamiko ya jinai dhidi ya Ramaphosa, akimtuhumu kwa kufanya makosa katika kujaribu kuficha wizi wa dola milioni 4 (pauni milioni 3.25) pesa taslimu katika shamba lake la wanyama pori kaskazini-mashariki mwa jimbo la Limpopo.

Ramaphosa amekana kufanya makosa yoyote akidai kuwa pesa hizo zilitokana na mauzo ya nyati katika shamba lake.

Kashfa hiyo ya muda mrefu imekuwa tatizo la kisiasa kwa Ramaphosa, huku vyama vya upinzani vikimtaka ajiuzulu.

Mwaka wa 2022 chama cha Rais Ramaphosa kilizuia kuundwa kamati ya kumuondoa madarakani kwa ajili ya kuchunguza zaidi tukio hilo, ambalo lilizua maswali kuhusu namna Ramaphosa alivyopata kiasi hicho kikubwa cha fedha na kwa nini, aliziweka kwenye samani badala ya benki.