Sababu Gani Zinaifanya UAE Ishupalie Vita Dhidi ya Iran?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i138216-sababu_gani_zinaifanya_uae_ishupalie_vita_dhidi_ya_iran
Muungano wa Falme za Kiarabu, UAE au Imarati umechukua msimamo wa waziwazi wa kushupalia vita hususan dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-05-06T11:34:15+00:00 )
May 06, 2026 11:21 UTC
  • Sababu Gani Zinaifanya UAE Ishupalie Vita Dhidi ya Iran?

Muungano wa Falme za Kiarabu, UAE au Imarati umechukua msimamo wa waziwazi wa kushupalia vita hususan dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Imarati ni nchi ndogo yenye eneo la chini ya kilomita za mraba 84,000 na idadi ya watu wapatao milioni 11, akthari yao wakiwa ni wageni. Nchi hiyo ndogo ya kifalme ina uchumi imara, lakini kwa upande wa kijeshi na kiusalama, ni taifa tegemezi linaloyategemea madola ya kigeni, hususan Marekani. Pamoja na hayo, licha ya changamoto ambazo serikali ya Imarati imekabiliana nazo katika miaka ya hivi karibuni kupitia mikwaruzano iliyozuka baina yake na Saudi Arabia juu ya suala la kujijengea satua na ushawishi katika Ulimwengu wa Kiarabu na katika nchi za bara la Afrika; na baina yake na Iran katika uga wa eneo la kijiografia, Abu Dhabi imeshirikiana pia na Washington na Tel Aviv katika vita vya kichokozi vya siku 40 vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hivi karibuni imeripotiwa kuwa, Muungano huo wa Falme za Kiarabu umeiomba Marekani ianzishe tena vita dhidi ya Iran; na serikali ya Abu Dhabi kwa upande wake, itagharimia vita hivyo kifedha. Kwa hiyo, suali linalojitokeza hapa ni: Sababu gani zinaifanya Imarati ishupalie vita dhidi ya Iran? 
Inavyoonekana, kuna majibu mawili yanayoweza kutolewa kwa suali hili. Jibu la kwanza ni kwamba, Imarati inafuata zaidi mdundo wa ngoma ya Israel; yaani inavyohisi nchi hiyo, umuhimu wake kwa utawala wa Kizayuni ni mkubwa kuliko umuhimu wake kwa Marekani. Inavyoamini Abu Dhabi ni kwamba ikiwa itafuata mdundo wa ngoma inayopigwa na utawala wa kizayuni, itaungwa mkono na utawala huo ghasibu, ambapo mbali na kunufaika na uwezo wa aina mbalimbali ilionao Israel hususan katika uga wa teknolojia, itapata uungaji mkono wa Tel Aviv pia kwa ajili ya kupanua satua na ushawishi wake wa ndani na nje ya eneo na katika kukabiliana na vitisho vya nje.

Kwa hiyo, chokochoko zinazofanywa hivi sasa na Imarati za kuchochea moto wa vita dhidi ya Iran zinaweza ikawa zinafanywa kwa wito wa utawala bandia wa Israel au yakawa ni matokeo ya mtazamo ilionao Abu Dhabi kuhusiana na Tel Aviv. 
Lakini jibu la pili linahusiana na hisia za uelewa ilizonazo Imarati kwa nafasi na maslahi yake. Katika miongo ya karibuni nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi imezidi kuwa mpenda makuu na yenye matarajio makubwa katika uga wa sera zake za nje kwa sababu ya ghururi iliyotokana na ukuaji mkubwa wa uchumi wake. Kuhusiana na hilo, Imarati ishakwaruzana na Saudi Arabia katika nyuga tofauti, ilichukua hatua dhidi ya Qatar mwaka 2017, ikavutana pia na Uturuki, na imekuwa ikirudia mara kwa mara madai ya ardhi ya umiliki wa visiwa vya Iran. 
Hivi sasa pia, inavyoipitikia Imarati ni kwamba kwa kushiriki katika vita dhidi ya Iran, itapata fursa ya kufuatilia madai yake ya ardhi kwa uungaji mkono wa Marekani na utawala wa Kizayuni.
Lakini nukta yenye umuhimu hapa ni kwamba, Imarati inafanya makosa ya kimahesabu na inapitikiwa na ufahamu potofu kwa kudhani, kwanza, itaweza kupata maslahi yake kwa kutegemea ubavu wa utawala wa Kizayuni, wakati Israel yenyewe haina uwezo wa kufanikisha maslahi yake bila msaada na uungaji mkono wa Marekani. Lakini pili ni kuwa, Israel ni utawala unaochukiwa mno katika eneo la Asia Magharibi na duniani kote, na kwa hiyo kuongezwa ushirikiano wa Imarati na utawala huo wa kizayuni kutaifanya Abu Dhabi, nayo pia ichukize katika eneo hili. Ni muhimu pia kuashiria hapa nukta hii, kwamba endapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaamua kutoa jibu kali kwa Imarati, uwezo wa kiusalama wa nchi hiyo, ni dhaifu kiasi ambacho kwamba, hasara itakayopata itakuwa kubwa mno.../