Hemedti atoa masharti kwa ajili ya kurejeshwa utulivu huko Sudan
Kamanda wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vya Sudan (RSF) ametaka kuuzuliwa kamanda wa jeshi la nchi hiyo ili kurejesha utulivu nchini humo.
Mapigano ya umwagaji damu yanaendelea huko Khartoum mji mkuu wa Sudan na katika miji mingine ya nchi hiyo kati ya jeshi la taifa linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na vikosi vya RSF vinavyoongozwa na Kamanda Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la "Hemedti" tangu katikati ya mwezi Aprili mwaka huu.
Juhudi za upatanishi wa kikanda na kimataifa kwa ajili ya kufikia mapatano ya kudumu ya kusitisha vita huko Sudan hadi sasa hazijazaa matunda.
Mohamed Hamdan Dagalo jana alitangaza kuwa mapatano yanaweza kufikiwa nchini Sudan katika muda wa masaa 72 iwapo Abdel Fattah al Burhan kamanda wa jeshi la nchi hiyo atajiuzulu wadhifa huo.
Wakazi wa mji mkuu Khartoum wanaendelea kutaabika kutokana na matatizo mbalimbali hususan ongezeko la hali ya joto, kukatwa maji na huduma za umeme tangu kuanza mapigano kati pande mbili hizo.