Wahanga wa mauaji ya kimbari Rwanda wakosoa mwito wa mahakama ya UN
Waathirika, wahanga na manusura wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 wamekosoa vikali mwito uliotolewa na majaji wa rufaa ya mahakama ya Umoja wa Mataifa wa kutaka kesi ya uhalifu wa kivita inayomkabili mshukiwa wa mauaji hayo ya kimbari, Felicien Kabuga isitishwe kwa muda usiojulikana.
Francine Uwamariya, mmoja wa manusuru wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ameliambia shirika la habari la Associate Press kuwa, "Nahisi dunia haitutakii mema. Tulichotaka kwa uchache kama manusura wa mauaji ya kimbari baada ya kukamatwa Kabuga, ni haki."
Manusura mwingine wa mauaji hayo ya 1994, Naphatal Ahishakiye naye amesema inaelekea kuwa mahakama hiyo ya UN iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi iko upande wa wauaji, wakati ambapo ilipasa isiegemee upande wowote.
Ahishakiye ambaye ni Katibu Mtendaji wa Ibuka (umoja wa manusura wa mauji ya kimbari Rwanda) amebainisha kuwa, "Inasikitisha na kukera sana kwa upande wa manusura, kuona Kabuga anaachiwa huru. Waliokosewa walipasa kuhisi haki na uadulifu."
Juzi Jumatatu, Majaji wa Umoja wa Mataifa waliamuru kesi hiyo ya uhalifu wa kivita dhidi ya Kabuga mwenye umri wa karibu miaka 90 isitishwe kwa muda usiojulikana kwa sababu ana matatizo ya akili.
Ikumbukwe kuwa, mwezi Juni mwaka huu, majaji katika Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya Umoja wa Mataifa waliamua kuwa Felicien Kabuga hafai kufikishwa mahakamani kutokana na ugonjwa wa akili lakini walipendekeza taratibu mbadala zifanyike. Kwa sasa majaji wa rufaa wamekataa pendekezo hili.
Kabuga anatuhumiwa kueneza chuki na mauaji kupitia kituo chake cha redio na kuwahamasisha wauaji waliowaua zaidi ya watu 800,000 katika kipindi cha siku 100 tu. Alikamatwa mjini Paris mwaka 2020, baada ya miongo miwili ya kuwa mafichoni. Kabuga hata hivyo anakanusha mashtaka dhidi yake.