WHO: Asilimia 40 ya Wasudan wanasumbuliwa na njaa
Shirika la Afya Dunia (WHO) limetangaza kuwa, asilimia 40 ya wananchi wa Sudan wakabiliwa na baa la njaa.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dakta Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema katika kikao na waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, shirika hilo la Umoja wa Mataifa linatiwa wasiwasi na hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili Sudan kutokana na mgogoro wa ndani ambao unaingia mwezi wake wa nne.
Amesema idadi ya watu wanaosumbuliwa na njaa nchini humo imeongezeka maradufu tokea Mei mwaka jana 2022. Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watu milioni 6 wako kwenye ukingo wa mwisho wa janga kubwa la njaa nchini Sudan.
Mashirika ya misaada ya kibinadamu yameonya kuwa Sudan, ambayo hivi sasa imezama kwenye dimbwi la vita vya wenyewe kwa wenyewe vya majenerali wa kijeshi, iko katika hatari ya kuenea magonjwa hatari kwani maelfu ya miili ambayo haijazikwa imeachwa ikizagaa mitaani, huku na miundombinu ya afya ya nchi hiyo imesambaratishwa.
Takriban watu 3,900 wanahofiwa kuuawa nchini Sudan tangu vita baina ya majenerali hayo wa kijeshi vilipoanza tarehe 15 Aprili mwaka huu 2023.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR lilitangaza Jumanne iliyopita kwamba, zaidi ya watu milioni nne wamekimbia makazi yao nchini Sudan kutokana na mapigano hayo.