SADC, EU: Uchaguzi wa Zimbabwe umekumbwa na kasoro nyingi
Huku wananchi wa Zimbabwe wakiendelea kusubiri matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumatano iliyopita na kuendelea mpaka Alkhamisi, timu za uangalizi wa uchaguzi huo zimetilia shaka mwenendo wa zoezi hilo la kidemorasia, zikisisitiza kuwa uchaguzi huo umekumbwa na dosari na wizi za kura.
Waangalizi wa uchaguzi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wamekosoa mwenendo mzima wa uchaguzi nchini Zimbabwe ambapo kura zinaenendelea kuhesabiwa.
SADC imesema ingawaje upigaji kura ulikuwa wa amani, lakini baadhi ya vipengele havikufuata sheria na miongozo ya uchaguzi ya nchi hiyo.
Kadhalika timu ya uangalizi wa uchaguzi ya Umoja wa Ulaya imesema mchakato mzima wa uchaguzi huo umekumbwa na dosari, ambapo haki za binadamu zimekiukwa, utumiaji wa mabavu, haki ya watu kukusanyika imekanyagwa, mbali na mikutano ya upinzani kuzuiwa kabla ya uchaguzi huo. EU imesema kasoro hizo zimeufanya uchaguzi huo kutokuwa wa huru na haki.
Hii ni katika hali ambayo, zaidi ya wasimamizi 40 wa kura walikamatwa na maafisa usalama wa nchi hiyo walipokuwa wakijaribu kujumuisha kura ambazo hazikupigwa na wananchi.
Huku hayo yakiarifiwa, mgombea wa chama kikuu cha upinzani katika uchaguzi wa rais nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa amesema zoezi hilo la wiki hii limekumbwa na kasoro nyingi na udanganyifu mkubwa, na kuna njama za kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo.

Chamisa amesema licha ya mizengwe kugubika zoezi hilo la kidemokrasia, lakini ana uhakika kwamba ushindi utakuwa wao. Amesema, "Kuna njama za kutupokonya ushindi, lakini tutaendelea kushinikiza kutolewa matokeo halali na yenye itibari ya uchaguzi huu."
Wananchi wa Zimbabwe waliotimiza masharti ya kupiga kura, mapema Jumatano walilekea katika vituo vya kupigia kura kushiriki uchaguzi huo utakaoamua iwapo Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa atashinda muhula wake wa pili na wa mwisho au la.
Kuna wagombea 11 wa urais katika uchaguzi huo, lakini mchuano mkali unatazamiwa kuwa baina ya Rais Mnangagwa (80) anayewania kupitia chama tawala ZANU-PF na Nelson Chamisa (45) wa Muungano wa Wananchi kwa ajili ya Mabadiliko (CCC).
Kamisheni ya Uchaguzi Zimbabwe (ZEC) imesema matokeo rasmi na ya mwisho ya uchaguzi huo yatatangazwa Jumatatu ijayo.